• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Dkt Mwangangi afafanua kuhusu kazi ya chanjo mwilini

Dkt Mwangangi afafanua kuhusu kazi ya chanjo mwilini

Na SAMMY WAWERU

CHANJO haizuii mtu kuambukizwa au kutoambukiza maradhi lakini inaimarisha kinga, imesema Wizara ya Afya.

Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Mercy Mwangangi alisema kuwa chanjo dhidi ya Covid-19 inaongeza na kupiga jeki kingamwili, ili kuepusha aliyepata kuhangaishwa na makali ya corona.

“Ningetaka kuweka wazi kuwa chanjo inayotolewa haizuii kuambukizwa au kutoambiza Covid-19. Inaongeza kinga mwilini ili unapopata virusi utakuwa imara,” Dkt Mwangangi akasema.

Ni kufuatia hilo ambapo Wizara ya Afya imewataka wananchi kuendelea kutii sheria na mikakati iliyopendekezwa kusaidia kuzuia maambukizi zaidi, licha ya chanjo ya AstraZeneca kuendelea kutolewa nchini.

Dkt Mwangangi amehimiza umma kuendelea kuvalia barakoa, kunawa mikono kwa sabuni au kuitakasa kwa jeli, kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake na kuepuka kukongamana.

Katika siku za hivi karibuni, kiwango cha maambukizi ya virusi vya corona kimeonekana kuongezeka kwa kasi.

Hadi kufikia sasa, Wizara ya Afya inasema imetoa chanjo kwa wahudumu wa afya, walimu na maafisa wa usalama wapatao 50,000.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini, Dkt Patrick Amoth alikuwa mhudumu wa afya wa kwanza nchini kupata chanjo hiyo.

Baada ya waliolengwa, Wizara ya Afya inasema itaanza kutoa chanjo kwa wazee waliofikisha umri wa miaka 58 na zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Wanne wajeruhiwa baada ya boti kugonga ukuta wa ufuo wa...

Wakenya waanza ndondi za Kinshasa vyema, mashindano...