• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Wanne wajeruhiwa baada ya boti kugonga ukuta wa ufuo wa bahari eneo la Mokowe

Wanne wajeruhiwa baada ya boti kugonga ukuta wa ufuo wa bahari eneo la Mokowe

Na KALUME KAZUNGU

WAFANYAKAZI wanne wa serikali ya Kaunti ya Lamu wamejeruhiwa boti ilipokosa mwelekeo na kugonga ukuta wa ufuo wa bahari eneo la Mokowe.

Ajali hiyo ya Jumatatu usiku ilitokea pale nahodha wa boti aliposhindwa kuidhibiti boti hiyo, hivyo kuishia kugonga ukuta huo wa ufuo wa Bahari Hindi kwa upande wa mbele.

Miongoni mwa walioumia kwenye ajali hiyo ni bawabu wawili waliokuwa wakielekea kwenye makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu mjini Mokowe ili kutwaa hatamu ya usiku.

Wengine ni mfanyakazi wa idara ya maji na nahodha wa boti hiyo.

Wote walipata majeraha ya kichwani, kifuani, mikononi na miguuni, hivyo kukimbizwa kwenye hospitali kuu ya King Fahad kisiwani Lamu kwa matibabu ya dharura.

Akithibitisha ajali hiyo, Afisa Msimamizi wa Kitengo cha Kukabiliana na Majanga, Kaunti ya Lamu Abdulaziz Luqman alisema watatu kati yao walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani ilhali mmoja ambaye ni mfanyakazi wa idara ya maji yuko katika hali mahututi hospitalini.

“Boti yenyewe ilikuwa imetoka hapa mjini Lamu ikielekea Mokowe kuwasafirisha wafanyakazi wanne wa serikali ya kaunti, lakini ikakumbwa na hitilafu wakati nahodha akijaribu kuisimamisha kwenye Jeti ya Mokowe,” akasema Bw Luqman.

Walioshuhudia tukio hilo aidha walimlaumu nahodha wa boti kwa kukosa umakinifu wakati akikaribia kusimamisha boti yake kwenye jeti hiyo ya Mokowe.

“Hata kama kulikuwa na hitilafu lakini pia nahodha alikuwa na utepetevu Fulani. Kwanza boti ilikuwa ikiendeshwa kwa kasi kupita kiasi. Hiyo ndiyo sababu boti ilifeli kusimama wakati nahodha akiwa amefika mahali pa kusimamia. Iligonga ukuta n ahata kuupanda juu. Tushukuru kwamba hakukuwa na vifo,” akasema Bw Ali Omar ambaye ni kibarua kwenye jeti hiyo ya Mokowe.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Boti na Mashua kisiwani Lamu, Hassan Awadh aliwataka manahodha wa boti kukagua vyombo vyaomara kwa mara kabla ya kuanza kuvitumia kwa shughuli za siku ili kuepuka maafa baharini.

“Ajali ilitokea baada ya boti kupata hitilafu. Cha msingi ni manahodha kuwa makini. Wakague boti zao kabla ya kuzitumia kwa shughuli za siku za kubeba wateja wao. Tukifanya hivyo hizi ajali za mara kwa mara zitapungua,” akasema Bw Awadh.

Februari 2020, mwanamke wa makamo alifariki ilhali wengine sita wakijeruhiwa pale mojawapo ya sehemu za injini ya boti hiyo ilipochomoka na kuwakatakata abiria hao.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Tusitiri huko Wiyoni, Lamu.

Oktoba, 2019, abiria watatu walinusurika kifo baada ya boti walimokuwa wakisafiria ilipogongana ana kwa ana na boti nyingine karibu na jeti ya Mokowe katika kisiwa cha Lamu.

You can share this post!

Uhuru asifu Pombe kwa kuhepa ukopaji

Dkt Mwangangi afafanua kuhusu kazi ya chanjo mwilini