• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
DOUGLAS MUTUA: Tuwasitiri na tuwapende wakimbizi wa Afghanistan

DOUGLAS MUTUA: Tuwasitiri na tuwapende wakimbizi wa Afghanistan

Na DOUGLAS MUTUA

TANGU hapo mcheka kilema hafi kabla hakijamfika. Ni tahadhari ya wahenga, lakini Mkenya ana mazoea ya kuipuuza.

Juzi Wakenya wamewacheka Waganda kwa kuwa Rais Yoweri Museveni ameidhinisha kimyakimya mpango wa kuwapokea wakimbizi 2,000 kutoka Afghanistan.

Kicheko hicho kilitokea kwa kuwa Waganda waliraukia habari hizo tukizi zilizosema kuwa Waafghani wanaweza kushuka uwanjani Entebbe wakati wowote.

Yaani hakuna hata ilani wala tahadhari kutoka serikalini, mzee Museveni aliamua kivyake tu na maaandalizi ya kuwapokea wakimbizi hao yakaanza.

Nusura mambo yaende visivyo kwani Rais Museveni mwenyewe alitaka iwe siri. Alimdokezea msiri wake ambaye hangeziba kinywa. Ilivuja!

Hata ni heri Waganda ambao walifikiwa na habari hizo za kushtukiza; Kenya tungali gizani, hatujui kunapangwa nini!

Labda mkataba ulishatiwa saini kitambo, tunawasubiri wakimbizi, ikiwa hawajaingia tayari, lakini hatuna mwao na mipango ya serikali yetu.

Labda mambo yamefanyika, nao wasiri wa watawala wetu wakafyata madomo ati. Labda kufumba na kufumbua utawaona usiowafahamu wakishuka ndege Nairobi.

Tuna hulka ya kutaka kuwapiku majirani zetu kwa kila tunachokifanya, hivyo ikiwa Waganda wanawapokea 2,000 huenda sisi ni maradufu au zaidi.

Kumbuka chochote kinaweza kutokea nchini Kenya; hata baadhi ya mikopo tunayopewa na Muungano wa Ulaya (EU); Benki ya Dunia na kadhalika hujulikana kwa bahati mbaya.

Na ukithubutu kufuatilia matumizi ya hela hizo unaambiwa una kiherehere sana, nao mamluki wa mitandaoni wanakuita mzembe mdaku, uiambie serikali ikupe kazi ati.

Kutokana na msukosuko wa kisiasa uliotokea Afghanistan baada ya waasi wa Taliban kuipindua serikali, Marekani imeyasihi mataifa kadha ya Afrika yawasitiri wakimbizi.

Kisa na maana ni kwamba wakimbizi wanaogopa kuuawa na makachinja wa Taliban ambao wana itikadi kali za kidini, hivyo wako radhi kutorokea kokote — hata Afrika.

Wanaohofia kuuawa hasa ni wasiopenda udini kwenye siasa na walioisaidia Marekani kwa vyovyote ilipowapiga vita Taliban nchini Afghanistan kwa miaka 20 iliyopita.

Kwa vile Marekani imejiondoa huko, serikali dhaifu ya Rais Ashraf Ghani imebanduliwa ghafla bila pingamizi, rais mzima akatorokea Arabuni! Mwingine nani asubiri?

Mbona Marekani isiwasitiri wakimbizi hao mara moja ilhali ilishirikiana nao wakati ambapo ilihitaji ushirikiano huo kikweli ili kuwashinda Taliban? Labda unauliza.

Hii ni dharura – watu wanakimbilia usalama wao – tena Marekani mambo hayafanyiki kwa pupa unavyodhani.

Umesikia ahadi ngapi za kulifunga gereza la Guantamano Bay, Cuba, walikofungwa watuhumiwa wa ugaidi?

Sheria za Marekani zimejenga mifumo imara yenye urasimu ambao hauwezi kuondolewa ghafla tu ili kwenda na majira; ni lazima ngano na magugu vichujwe kikamilifu kwanza.

Ni kwa mintaarafu hiyo ambapo Marekani imeyaahidi mataifa yaliyokubali kuwapokea wakimbizi hao kwamba yatawasitiri kwa muda wa miezi mitatu hivi suluhu ikitafutwa.

Kanuni za Umoja wa Mataifa zinazitaka nchi kuwa tayari kuwapokea na kuwasitiri watu wanaokimbia vita na manyanyaso.

Hii ina maana kwamba Uganda, Kenya na mataifa mengineyo duniani yana jukumu la kufanya hisani hiyo inayoonyesha imani kwa binadamu wenzetu walio hatarini.

Ni kitu kizuri kwa bara letu kupata fursa hiyo ya kuwatendea wema watu kutoka mabara mengine duniani, hata wale ambao hawakuwahi kuota wakizuru, acha kuishi, Afrika.

Waoga waitwao wahafidhina watakuogofya kwa kukwambia wageni hao watakuja na tamaduni na imani ngeni ambazo zitatishia za wenyeji.

Hayo ni mawazo finyu; mtagusano kati ya tamaduni tofauti hunogesha mahusiano na kuboresha tamaduni husika.

Wahafidhina wa kidini wakikwambia Waafghani wataleta Uislamu wao Afrika, wakumbushe dini hiyo ndiyo inayosambaa zaidi Afrika. Tena waliomo hawajamla mtu!

Tuwatendeeni wema wakimbizi na wanyonge wengineo wanaohitaji huruma na msaada; leo kwao, kesho kwetu. Mola na atuepushane na maafa.

[email protected]

You can share this post!

BBI ilivyotafuna mabilioni ya mlipa ushuru

WANDERI KAMAU: Amerika inavyotumia unafiki kuendeleza...