• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Familia 12,000 Mukuru zapoteza makao serikali ikiunda barabara mpya

Familia 12,000 Mukuru zapoteza makao serikali ikiunda barabara mpya

Na SAMMY KIMATU

ZAIDI ya watu 12,000 watakosa makao yao ili kubisha nafasi ya ujenzi wa barabara za lami na nyumba za kudumu zitakazokuwa za gharama ya chini.

Barabara hizo za lami zitakuwa za jumla ya urefu wa kilomita 3.2 na kuchukua nafasi ya ekari 4.4 za ardhi kwenye mitaa minne.

Aidha, jumla ya mitaa mitano ya mabanda katika wadi ya Nairobi Kusini na wadi ya Landi Mawe, kaunti ndogo ya Starehe imepangiwa kunufaika na maendeleo kupitia miundo msingi.

Akizungumza jana, mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were alisema serikali imetoa ilani ya watu kutoa nafasi kwa mradi huo ambao ni moja ya Ajenda Nne Kuu za rais uhuru Kenyatta.

Watakaohama makwao na kutafuta nyumba za kuishi kwingineko ni pamoja na wakazi katika mtaa wa mabanda wa Kaiyaba, Hazina, Fuata Nyayo, Mariguini na Commercial.

Bw Were alisema hayo wakati alipoongoza mkutano na maafisa wa Mamlaka ya Barabara za Jiji (KURA) na viongozi mbalimbali kutoka tarafa ya South B.

Kando na hayo, ofisa huyo wa utawala alitoa wito kwa wakazi kushirikiana na mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara sawia na atakayejenga nyumba.

“Serikali imetangaza kwamba mradi huu wa rais umechelewa kwa muda wa mwezi mmoja kwa hivyo ni lazima watu wapewe ilani mapema kabla ya kuondoka kutoka kwa nyumba na biashara zao,” Ofisa huyo wa utawala akanena.

Hata hivyo, aliongeza kwamba kutakuwa na mkutano mwingine kesho (Jumanne) ili wakazi washirikishwe.

Mkutano huo pia utakuwa katika makao makuu ya tarafa hiyo kwenye mtaa wa Hazina.

Mhandisi wa serikali Bi Jeniffer Korir alisema mradi huo unajulikana, “Upgrading to Bitumen Standard of Mariguini Housing Project Roads,” yaani kupandisha daraja hali ya barabara hili zifikie kiwango cha kuwekwa lami katika mradi wa Ujenzi wa Nyumba mtaani Mariguini.

Bi Korir alikariri kwamba serikali imelenga kubadilisha mtaa huo wa mabanda na kujenga nyumba badala za orofa ambazo ni za bei nafuu kwa minajili ya kuinua maisha ya wenyeji.

Afisa mwingine wa serikali kutoka kwa idara husika ya ujenzi wa Nyumba kwa jina Bw Muli alisema serikali ilikuwa awali imepima kutakojengwa barabara na kuchukua takwimu za watu watakaohamishwa.

”Mpango wa Kuinua Viwango vya Mitaa ya Mabanda Jijini ulianza kitambo ambapo idadi ya watakaotoa nafasi ya nyumba zao kupisha ujenzi wa barabara kuwa watu zaidi ya 2,000 watakaowacha nafasi ya jumla ya ekari 4.4 za ardhi kwenye mitaa husika,” Bw Muli asema.

Kwa mujibu wa Bw Were, serikali imesema zaidi ya asilimia 30 ya ardhi kaunti ya Nairobi imechgukuliwa na mitaa ya mabanda.

“Wakazi katika mitaa hiyo huishi maisha ya unyanyasaji wa matapeli na kila haina ya uhalifu huhusishwa na mitaa ya mabanda kulingana na utafiti wa serikali,” Bw Were akaambia Taifa Leo.

Vilevile, ripoti ya serikali, kulingana na Bw Were ni kwamba jiji la Nairobi ni miongoni mwa miji mingine iliyo na mitaa mingi ya mabanda ulimwenguni jambo llinalolishusha hadhi yake kimataifa.

You can share this post!

Mbunge aalipa dhamana ya Sh100,000 kwa kumcharaza msanii

Washtakiwa wenza wa Mbunge Rigathi Gachagua wakana ufisadi...