• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Familia ya msanii aliyefariki baada ya kupigwa akitoka kutumbuiza yalilia haki

Familia ya msanii aliyefariki baada ya kupigwa akitoka kutumbuiza yalilia haki

CECIL ODONGO na JOHN NJOROGE

FAMILIA ya msanii chipukizi Kevin Maina inalilia haki kutokana na mauti yake ya kutatanisha wiki iliyopita.

Marehemu Maina, 25 alizikwa kwenye shamba la babake la Nyakiambi, Elburgon, eneobunge la Molo mnamo Alhamisi wiki hii. Aliaga dunia kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya watu waliomtuhumu kuwa mwizi kumpiga vibaya usiku wa Septemba 28.

Alikuwa asafiri  Jumatatu hii kuanza kazi kama mhudumu kwenye hoteli kule Qatar pamoja na kuendeleza talanta yake ya uimbaji.

Kwa mujibu wa babake, Peter Njoroge Wang’ombe, mwanawe alipigwa na kujeruhiwa nje ya lango la nyumba wanakoishi mtaani Umoja Innercore Nairobi. Maina, alikuwa ametoka kupiga shoo na alirejea nyumbani usiku mkuu alipokumbana na madhila hayo.

“Siwezi kuamini kuwa mwanangu ameaga dunia. Wale ambao waliimuua hawatakuwa na amani na nitahakikisha kuwa familia yangu imetendewa haki,” akasema Bw Njoroge, 47 machozi yakimtoka njia mbili.

Bw Peter Njoroge aonyesha mwanahabari wa Nation picha ya marehemu kijana wake Kevin Maina Njoroge aliyefariki akiwa na umri wa miaka 25 jijini Nairobi na kuzikwa nyumbani Nyakiambi Farm mjini Elburgon katika Kaunti ya Nakuru mnamo Oktoba 13, 2023. PICHA | JOHN NJOROGE

Kevin alikuwa msanii ambaye alikuwa akiibukia kwa kasi na alikuwa akishiriki shoo nyingi ikiwemo 10 over 10 na pia One Love ambazo ni maarufu sana kwenye runinga ya Citizen.

Waliomvamia Maina ambaye alikuwa maarufu kama ‘King Dyce’ usiku wa tukio walishikilia kuwa alikuwa mshirika wa mhudumu wa bodaboda  aliyekuwa amewaibia. Walimpiga na kumwaacha na jeraha baya la kichwa huku Bw Njoroge na baadhi ya wanaoishi karibu nao wakitoka na kumwokoa.

“Walipomkosa mwendeshaji wa bodaboda, walimfikia mwanangu na kumwaangushia kipigo wakisema alikuwa naye. Niliamshwa na mmoja wa wapangaji na tukaenda kumwokoa huku vijana ambao walikuwa wakimpiga wakihepa,” akasema Bw Njoroge ambaye ni mjane kwa kuwa alifiwa na mke wake miaka kadhaa iliyopita.

Alikumbatia mchakato wa kuyaokoa maisha mwanawe. Huku akisaidiwa na jirani yake, walimkimbiza hasi hospitali ya Mama Lucy. Waliamrisha wamfikishe Hospitali ya Kenyatta kwa kuwa alikuwa na majeraha mabaya hasa kichwani yaliyohitaji matibabu maalum.

Baada ya hali yake kuimarika kidogo, babake anasema alimrejesha nyumbani mnamo Oktoba 3. Hata hivyo, mambo yaligeuka na hali yake ikawa mbaya ndipo akamrejesha Kenyatta ambako aliaga dunia mnamo Oktoba 5, 2023.

Bw Peter Njoroge, akiwa kando ya kaburi la kijana wake Kelvin Maina Njoroge, 25, katika shamba lake eneo la Nyakiambi, Elburgon, Kaunti ya Nakuru mnamo Oktoba 13, 2023. PICHA | JOHN NJOROGE

“Uchunguzi wa upasuaji wa maiti ulionyesha kuwa fuvu la kichwa cha mwanangu lilikuwa limeharibiwa vibaya. Mwanangu hakuwa mwizi na kwa miaka minane ambayo tumeishi naye hapo, sijawahi kuarifiwa ana kesi yoyote dhidi ya mtu,” akasema.

Alipiga ripoti kuhusu mwanawe kupigwa mnamo Septemba 29 kwenye Kituo cha Polisi cha Buruburu kisha alirejea Jumatatu hii baada ya mauti yake. Bw Njoroge anasema kuwa waliomuua mwanawe wanajulikana na mmoja wao ambaye alikuwa akiishi hapo karibu alihama baada ya kupata habari alikuwa akiandamwa.

“Waliompiga walipiga ripoti kuwa walikuwa wameibiwa. Polisi walifika na kuwakamata baadhi ya vijana ambao walikuwa wanawaandama waliompiga na wanaendelea kuzuliwa kwenye Gereza la Industrial Area. Hata hivyo, hao hawana hatia na ni vyema waachiliwe,” akasema.

Afisa wa cheo cha Inspekta kwenye Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) Buruburu  Emmanuel Kipkogey alisema wanaendelea na uchunguzi na lazima familia itapata haki. Alifichua kuwa baada ya kumaliza uchunguzi watawanyaka wale ambao walikuwa wamepiga ripoti kuhusu kuibiwa kwa kuwa ndio walimpa Kevin kipigo kilichosababisha mauti yake.

“Nahakikishia familia kuwa haki itapatikana. Kwa sasa tunaendelea na uchunguzi na washukiwa watapelekwa kortini baada ya shughuli hiyo kukamilika,” akasema Bw Kipkogey.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge Alice Ng’ang’a asema Thika Mjini isipogawanywa...

Serikali kutumia Sh90 bilioni kukwamua vyuo vikuu

T L