• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:36 AM
Gachagua atimiza ahadi ya mchele na nyama kwa wakazi Mlima Kenya, asema pia ya uji yaja

Gachagua atimiza ahadi ya mchele na nyama kwa wakazi Mlima Kenya, asema pia ya uji yaja

NA MWANGI MUIRURI 

HATIMAYE ahadi ya Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ya kuwatuza wenyeji wa Mlima Kenya mlo wa wali, nyama na viazi kama mradi wa kimaendeleo ndani ya Ikulu ndogo ya Sagana ilitimia Jumapili, Agosti 6, 2023.

Akifanya kampeni za urais mwaka jana, 2022 ambapo alikuwa akimuunga mkono mwaniaji wa urais Dkt William Ruto – na wakaibuka washindi, Bw Gachagua alikuwa amesema kwamba “tukichukua hii serikali tutakuja kuwaonyesha jinsi ya kuwatuza mlo halisi….Huyu Uhuru Kenyatta akiwaita huko anawapea soda na mkate kama watoto wa shule”.

Alisema Ikulu ni mahali ambapo watu wanapaswa kula vizuri, akisema wali na nyama ndio kula.

Baadhi ya wakazi wakipanga laini kupakuliwa nyama na mchele katika Ikulu ndogo ya Sagana mnamo Jumapili, Agosti 6, 2023 kwa mujibu wa ahadi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua. Picha|MWANGI MUIRURI 

Mnamo Jumapili ambapo Rais William Ruto aliye katika ziara ya siku tano, aliongoza ushirika wa ibada ya pamoja, waliofika kwanza walituzwa mlo uliofana.

“Leo ni Leo…Asemaye hatujafika Ikulu kama tulivyotamani ni nani? Tuko hapa tule pamoja na Rais wetu tuliyejichagulia kwa hiari. Tumefika hapa kumkaribisha maskani hii yake ambayo itakuwa himaya yake ya heshima hadi 2032,” akasema Bw Gachagua.

Alisema kwamba Ikulu hiyo ndiyo “walikuwa wakipanga njama za kudhalalisha ari ya Dkt Ruto ya kuwa Rais na kunipangia jinsi ya kukamatwa kila Ijumaa na kuachiliwa Jumatatu “.

Akaongeza: “Lakini kwa kuwa Mungu hali sima au kuwa na makao yake Kayole kama sisi binadamu wa kawaida alitujaalia ushindi na sasa ndio sisi hapa…Tule tunywe kwa shangwe”.

Baadhi ya wakazi Mlima Kenya wakishabikia wali; nyama na mchele katika Ikulu ndogo ya Sagana mnamo Jumapili, Agosti 6, 2023. Picha|MWANGI MUIRURI

Wapishi walikuwa wamekesha katika Ikulu hiyo huku nyama na mchele zikitua kwa malori.

Maafisa wa usalama walisema waliotuzwa mlo huo walikuwa takriban 30, 000.

Aidha, Bw Gachagua alikuwa ameahidi kujenga boma ndogo katika Kijiji cha Konyu kilichoko katika eneo hilo la Mathira.

“Walikuwa wameshika pesa yangu takriban Sh200 milioni. Niliahidi kwamba nikiipata baada ya kushinda uchaguzi ningerejea nijenge nazo boma la kujivinjari. Bado nakumbuka,” akasema.

Bw Gachagua aidha alisema watu wa Mathira watamkosa kwa kuwa akiwa mbunge alikuwa akichanga viwango vya juu katika hafla za harambee.

“Mimi nilikuwa na mali kwa kuwa nililima zamani. Nilikuwa nikichanga kati ya Sh50, 000 na Sh300, 000 na zaidi…Lakini huyu Eric wa Mumbi ambaye alirithi ubunge kutoka kwangu hajalima kama mimi. Akileta Sh2, 000 ninyi chukueni na msimpige vita…Atapata pia kama Mimi,” akasema.

Baadhi ya wakazi Mlima Kenya wakishabikia wali; nyama na mchele katika Ikulu ndogo ya Sagana mnamo Jumapili, Agosti 6, 2023. Picha|MWANGI MUIRURI

 

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Raila atishia kufufua maandamano ampa Ruto siku 30

Makahaba wakongwe na wachanga Thika wazozania bei na wateja

T L