• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:35 PM
Makahaba wakongwe na wachanga Thika wazozania bei na wateja

Makahaba wakongwe na wachanga Thika wazozania bei na wateja

NA MWANGI MUIRURI

MZOZO kati ya makundi mawili ya makahaba Thika umetokota, yakisemekana kuzozania bei ya huduma wanazotoa.

Mvutano huo unajumuisha makahaba wakongwe na wale wachanga, duru zikiarifu pia wanavutania wateja.

Msemaji wa makahaba wakongwe Bi Virginia Ngugi alisema kwamba wale wachanga wana tabia za kuibia wateja na pia kutoza ada za juu, hivyo basi kuwafanya wanaume kususia mji huo.

“Tuna makubaliano kwamba ada ziwe Sh200 kwa huduma ya muda mfupi, lakini hawa wasichana wadogo wanadai walipwe Sh500. Aidha, hata wakishalipwa hizo pesa za juu, wanawapora wateja pia,” akasema.

Hata hivyo, wasichana hao wadogo wamesema kwamba “mwili mzee hauwezi kuwa na bei moja na ule mchanga”.

Bi Faith Kagendo 19, alisema kwamba yeye hutoza Sh500 kwa huduma ya muda tu na huwa na wateja ambao hata humpa Sh1, 000.

“Hii ni biashara ya kurushana roho na raha ni joto, spidi na ustadi…Wakongwe wetu wa rika la mama na nyanya zetu wanataka tuuze huduma zetu sawa na zao baridi, dhaifu na legevu,” akasema Bi Kagendo.

Hata hivyo, Bi Ngugi alisema kwamba biashara yoyote haramu ni lazima iwe na umafia wa kuidhibiti.

“Ni lazima tuwe na nembo yetu ambayo inadhibitiwa na usawa wa bei, nidhamu ya kutunza soko letu kupitia kujiepusha na visa vya wizi na la mno, tuwe watiifu katika kutoa ada kuwapa maafisa wa polisi ili watunusuru wanapotekeleza misako,” akasema Bi Ngugi.

Alisema polisi hudai Sh50 kwa kila kahaba kwa siku.

Bi Kagendo alimtaka Bi Ngugi awapange wakongwe wake na akome kuingilia biashara ya vipusa.

“Thika ni yetu sote. Mali ni ya mtu binafsi na hakuna kulazimishwa jinsi ya kuigawia wateja. Ikiwa hajui, kuna wateja wengine ambao tunawapa bonasi ya kuburudika bure kwa kuwa hututunza vizuri. Endeni mkasikie vibaya na huko na mkilemewa na mbio mstaafu,” akasema.

Naibu Kamishna wa Thika Magharibi Bi Philomena Nzioki alisema kwamba “Tumechoka na haya madai ya kipuuzi kwamba maafisa wetu huchukua hongo kutoka kwa wakora hao”.

Alidokeza kuwa kila siku misako hutekelezwa dhidi ya wanawake hao na huwa wanatiwa mbaroni.

Hata hivyo, afisa huyo alisema wakuu wa kiusalama eneo hilo wako tayari kupashwa ushahidi wa ufisadi huo na hatua itachukuliwa.

“Wawe ni wakongwe au ni wachanga, cha kuelewa ni kwamba ukahaba ni biashara haramu hapa nchini na misako itaendelea tu hadi tustaarabike sote. Kile tu hatuulizi ni hali za kuchumbiana,” akasema.

Aliwataka wanaume wote ambao watajipata wakishinikizwa kushiriki ukahaba wapige ripoti katika kituo cha polisi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Gachagua atimiza ahadi ya mchele na nyama kwa wakazi Mlima...

Hakimu atoa onyo kwa walanguzi wa mihadarati na wagema...

T L