• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Raila atishia kufufua maandamano ampa Ruto siku 30

Raila atishia kufufua maandamano ampa Ruto siku 30

NA SAMMY WAWERU

KINARA wa Azimio la Umoja – One Kenya Raila Odinga ametishia kufufua maandamano, akisema serikali ya Kenya Kwanza haijaashiria kuangazia masuala yaliyoibuliwa na upinzani.

Akizungumza Jumamosi, Agosti 5, 2023 katika hafla ya mazishi ya mfuasi wa Azimio aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano, Siaya, Bw Odinga alisema endapo Rais William Ruto hataangazia changamoto zinazokumba Wakenya hatakuwa na budi ila kuitisha maandamano mwezi Septemba.

Kiongozi huyo wa upinzani aidha amempa Dkt Ruto makataa ya siku 30.

“Tunawapa mwezi mmoja, la sivyo tutarejelea maandamano,” Odinga akasema.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alisitisha maandamano kwa muda, katika kile alihoji ni “kuomboleza waliouawa wakati wa maandamano”.

Pande zote mbili; Azimio na mrengo tawala wa Kenya Kwanza, zimezindua wawakilishi watakaoshiriki mazungumzo ya mapatano.

Hii ni mara ya pili makundi ya aina hiyo kuzinduliwa kujaribu kuleta mwafaka.

Jaribio la kwanza mapema 2023, liligonga mwamba Azimio ikilalamikia Kenya Kwanza kukosa kujitolea kuangazia masusala yaliyoibuliwa na upinzani.

Bw Odinga hata hivyo amehakikisha kuwa tayari kwa mazungumzo.

Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Ruto unadai anachosaka Odinga ni handisheki na serikali ya nusu mkate.

“Mimi sitabembembeleza Raila Odinga. Wakati wa utawala wa Mzee Daniel Arap Moi alimsumbua akapewa kitu, Mwai Kibaki akagawiwa serikali na Uhuru Kenyatta, handisheki. Ninamwambia hakuna serikali ya nusu mkate wala handisheki,” Rais Ruto akasema mnamo Jumamosi katika ziara yake eneo la Mlima Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti zatenga pesa chache za bima ya afya

Gachagua atimiza ahadi ya mchele na nyama kwa wakazi Mlima...

T L