• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Gathoni Wamuchomba asifiwa kwa kupinga Mswada wa Fedha

Gathoni Wamuchomba asifiwa kwa kupinga Mswada wa Fedha

NA CHARLES WASONGA

WAKENYA katika mitandao ya kijamii wamemmiminia sifa Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba kwa kupinga Mswada wa Fedha wa 2023 Bungeni mnamo Jumatano.

Mbunge huyo anayehudumu muhula wake wa pili ndiye mbunge wa kipekee wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na muungano wa Kenya Kwanza, aliyekaidi agizo la Rais William Ruto na kuupinga mswada huo.

Bi Wamuchomba ni miongoni mwa wabunge 81, wengine wao wakiwa wale wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, waliopinga mswada huo ulipopigiwa kura baada ya kujadiliwa kwa hatua ya pili Bungeni.

Hata hivyo, mswada huo ulipitishwa katika hatua hiyo baada ya jumla ya wabunge 176 kupiga kura ya NDIO.

Wabunge wa mrengo tawala wa Kenya Kwanza walipigwa jeki na baadhi ya wabunge waasi wa Azimio.

“Mbunge huyu amefanya jambo la maana zaidi. Ndiye mzalendo halisi. Asante Mheshimiwa Wamuchomba kwa kusimama na wananchi wa kawaida licha ya vitisho kutoka kwa serikali,” Rein akasema kupitia Twitter.

Mbunge huyo pia amemfurahisha Sholla Adam aliyempongeza kwa kuamua kusimama na wabunge wachache waliopinga mswada huo. Kwa kufanya hivyo, anasema, Bi Wamuchomba anawakilisha sauti za idadi kubwa ya Wakenya.

“Asante kwa kuongea kwa niaba ya watu. Wa Muchomba ameelezea, kwa ujasiri, hisia za idadi kubwa ya Wakenya. Mungu akubariki,” Adam akasema.

Naye mwanaharakati Gabriel Oguda akasema: “Gathoni Wamuchomba ndiye Mwanamke Shupavu kutoka Mlimani. Amehiari kuadhibiwa na Ruto akitetea raia wa kawaida.”

Wakati wa mjadala kuhusu mswada huo Bungeni mnamo Jumatano, Bi Wamuchomba alisema wazi kuwa mswada huo utawaumiza watu wake wa Githunguri na Wakenya kwa ujumla.

“Watu wangu hawawezi kumudu lishe moja kwa siku. Gharama ya maisha iko juu zaidi. Bei ya unga iko juu zaidi,” akasema Bi Wamuchomba.

“Watu wangu wameniambia kuwa mswada huu ni dhalimu na kandamizi. Utawaongezea mzigo mkubwa wa ushuru ilhali tayari wamezongwa na kupanda kwa gharama ya maisha. Kwa hivyo, kwa masilahi ya jamii na utawala wa haki, ninapiga kura ya LA,” akasema Bi Wamuchomba huku akisifiwa na wabunge wa Azimio na kuzomewa na wale wa Kenya Kwanza.

Mapema mwezi huu wa Juni, Rais William Ruto alitishia kuwaadhibu wabunge wa Kenya Kwanza ambao watadiriki kuupinga mswada huo.

Hata hivyo, hakufafanua aina ya adhabu hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Eric Omondi aenda Uingereza na kugeuka ombaomba barabarani,...

Wakazi waparamia tembe za PEP na PrEP kuhepa kondomu...

T L