• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Gavana Nyoro atangaza mpango wa kuboresha viwanda Kiambu

Gavana Nyoro atangaza mpango wa kuboresha viwanda Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ya Kaunti ya Kiambu imefanya ushirikiano na mashirika ya bara la Ulaya ili kuzindua viwanda kadha vya kuwafaa wakazi.

Wakati huo huo pia kaunti ya Kiambu ina matarajio kwamba mji wa Kiambu utapandishwa hadhi.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema ujumbe kutoka benki ya European Development Bank utazuru Kaunti ya Kiambu mnamo Januari 14, 2022, ili kuafikiana kuhusu mipango hiyo.

Iwapo mkataba wa makubaliano utaafikiwa, Kaunti ya Kiambu inapanga kujenga viwanda kadha kama cha ngozi, cha uchakataji chakula cha mifugo, kiwanda cha nguo, na pia cha uchakataji wa nyama ya nguruwe.

Alieleza kuwa iwapo viwanda hivyo vitajengwa Kiambu, bila shaka vijana wengi watapata ajira na maendeleo kamili yatashuhudiwa.

“Kwa wakati huu kuna mambo mengi yanayostahili kutekelezwa kwa sababu Kaunti ya Kiambu ina idadi kubwa ya wakazi na kwa hivyo inahitaji maendeleo kwa wingi,” alifafanua gavana Nyoro.

Alieleza kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu Kiambu wataongeza manispaa nyingine sita ili kutosheleza matakwa ya wakazi wa hapo kimaendeleo.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa wiki jana wakati wa uzinduzi wa gari spesheli la zimamoto litakalosaidia kukabiliana na matukio ya moto katika eneo la Thika, na vitongoji vyake.

Alisema gari hilo la zimamoto lina uwezo wa kurusha maji lita 10,000 kwa muda wa dakika sita pekee.

Maeneo mengine yatakayopokea magari ya zimamoto ni Githunguri, Limuru, Githunguri, Kikuyu, na Uplands.

Alisema afisi yake tayari imetenga takribani Sh120 milioni za kuweka taa za barabarani katika kaunti ya Kiambu.

Alieleza hospitali kadha zimepanuliwa na kuwekwa vitanda vya kutosha wagonjwa.

Alisema barabara nyingine ya kutoka Thika hadi Ngoliba ya kilomita 20 inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Alieleza kuwa chini ya miezi minane ijayo, Kaunti ya Kiambu itakuwa imefanya maendeleo makubwa.

  • Tags

You can share this post!

Mama awadunga wanawe kisu, mmoja afariki

WANDERI KAMAU: Amerika, Ulaya zijue shida za kiusalama ziko...

T L