• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Hatutaruhusu wawaniaji wasio na digrii – ODM

Hatutaruhusu wawaniaji wasio na digrii – ODM

Na GEORGE ODIWUOR

CHAMA cha ODM kimeunga mkono sheria inayotaka wagombea wa udiwani wa ubunge kuwa na shahada ya digrii.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi jana alisema kuwa chama hicho hakitaruhusu yeyote kuwania bila kuwa na digrii ya Chuo Kikuu.Bw Mbadi alidai kwamba baadhi wanasiasa walipuuzilia mbali ushauri wake wa kuwataka kujiendeleza kimasomo baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Alidai kuwa wanasiasa waliopuuza ushauri wake ndio wanashinikiza sheria inayotaka madiwani na wabunge kuwa wamehitimu shahada ya digrii.Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen amesema kuwa ameandaa mswada wa kutaka kurekebisha Kifungu cha 22 cha Sheria za Uchaguzi kinachotaka wawaniaji wa kuanzia udiwani hadi rais kuwa na digrii.

Sheria hiyo haikutekelezwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita baada ya wabunge kupitisha hoja ya kutaka ianze kutekelezwa kuanzia 2022.Katika uchaguzi uliopita, ni wawaniaji wa urais, naibu rais, magavana pamoja na manaibu wao walitakiwa kuwa na digrii.

Lakini mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alitangaza kuwa ni sharti wawaniaji wanaotaka kuwania viti 2022 wawe na shahada ya digrii.Bw Murkomen anataka mwaniaji awe na uwezo wa kuandika na kusoma kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili au wawe wanafahamu lugha ya ishara kwa wasiosikia ama kuzungumza.

Bw Mbadi alisema kuwa pendekezo hilo la Bw Murkomen linafaa kutupiliwa mbali kwani linalenga kurudisha nyuma Wakenya.“Tunaweza kujadiliana kuhusu pendekezo kwamba madiwani wawe wamehitimu angalau cheti cha diploma.

Lakini pendekezo kwamba mwaniaji awe anajua kusoma au kuandika tu hatutakubali. Hatuwezi kuwa na watu ambao hawakufika hata Darasa la Nane ambao watatwikwa jukumu la kusimamia mabilioni ya fedha,” akasema.Kulingana na Bw Mbadi, wengi wa wabunge wanaohudumu sasa hawajui majukumu yao.

Mbunge wa Suba Kusini alisema kuwa wengi wa wabunge wanaenda katika mikutano ya kamati za Bunge kutia saini stakabadhi ya kutaka kupewa marupurupu ya kuhudhuria vikao na kisha kuondoka bila kuchangia mijadala.

“Changamoto kama hiyo pia iko katika mabunge ya kaunti ambapo mawaziri wa kaunti wasomi wanaenda kujibu maswali ya madiwani wasiokuwa na digrii.“Wengi wao wanakwepa hata kuuliza maswali kwa sababu hawaelewi kinachoendelea,” akasema Bw Mbadi alipokuwa akizungumza katika kituo kimoja cha redio.

Alisema chama cha ODM kitafuata sheria kwa kuhakikisha kuwa wanaoruhusiwa kuwania viti mbalimbali wana cheti cha digrii.

  • Tags

You can share this post!

Haji asihofie ugumu wakazi, aendelee kujitahidi

Mpango wa Tottenham kuajiri kocha Julen Lopetegui wa...