• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Mpango wa Tottenham kuajiri kocha Julen Lopetegui wa Sevilla wazaa nunge

Mpango wa Tottenham kuajiri kocha Julen Lopetegui wa Sevilla wazaa nunge

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

JUHUDI za Tottenham Hotspur kujinasia maarifa ya kocha Julen Lopetegui wa Sevilla zimeambulia pakavu baada ya ofa yao kukataliwa na mkufunzi huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uhispania.

Kwa mujibu wa Jose Castro ambaye ni rais wa Sevilla, Lopetegui hana mpango wowote wa kuagana na waajiri wake wa sasa hivi karibuni.Spurs wamekuwa wakitafuta kocha wa kurithi mikoba ya Jose Mourinho aliyetimuliwa mnamo Aprili 19, 2021.

Lopetegui, 54, aliongoza Sevilla kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) katika nafasi ya nne mnamo 2020-21 na hivyo kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).“Lopetegui alipokea ofa ambayo hakutaka hata kuisikiliza. Alinipigia simu na kunielezea kila kitu jinsi alivyoambiwa na Spurs,” akasema Castro.

“Makocha wengine hutawaliwa na msukumo wa kifedha. Lakini Lopetegui ameshikilia kwamba anafurahia maisha yake hapa. Tuna imani kubwa naye, ndiposa tukarefusha kipindi cha kuhudumu kwake kambini mwa Sevilla kwa miaka miwili zaidi,” akaongeza Castro.

Spurs walikamilisha kampeni zao za msimu wa 2020-21 chini ya kocha mshikilizi Ryan Mason ambaye alikuwa mkufunzi wao wa akademia. Antonio Conte aliyeagana na Inter Milan baada ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) alikuwa pazuri zaidi kupokezwa mikoba ya Spurs ambao pia waliazimia kumrejesha Mauricio Pochettino kwa kumng’oa kutoka Paris Saint-Germain (PSG.)

Kutibuka kwa mipango ya kuajiriwa kwa Conte na Pochettino kuliwafanya Spurs kumvizia aliyekuwa kocha wa AS Roma, Paulo Fonseca ambaye pia alikosa kuafikiana na usimamizi wa kikosi hicho. Spurs walihusishwa pia na uwezekano wa kuajiri kocha Gennaro Gattuso aliyeagana na Fiorentina baada ya siku 23 pekee.

Jurgen Klinsmann ambaye amewahi kunoa timu ya taifa ya Ujerumani na Amerika pamoja na vikosi vya Bayern Munich na Hertha Berlin amefichua kiu ya kudhibiti mikoba ya Spurs.

  • Tags

You can share this post!

Hatutaruhusu wawaniaji wasio na digrii – ODM

Uhispania kumenyana na Croatia katika 16-bora baada ya...