• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Hawa ni wezi wa watoto katika hospitali ya Mama Lucy, mahakama yathibitisha

Hawa ni wezi wa watoto katika hospitali ya Mama Lucy, mahakama yathibitisha

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI wawili katika idara ya huduma za kijamii ya hospitali ya Mama Lucy Kibaki, Nairobi wamepatikana na hatia ya ulanguzi wa watoto wachanga miaka mitatu iliyopita.

Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Milimani Bi Esther Kimilu aliwapata na hatia Fred Leparan na Selina Awuor Adunda ya ulanguzi wa watoto.

Bi Kimilu alisema upande wa mashtaka umethibitisha kabisa Leparan na Awuor walikula njama za kuwauza watoto wa umri mdogo kati ya wiki tatu na mwezi mmoja.

Hakimu aliwapata na hatia wawili hao kwa kula njama za kuwaiba watoto na kuwauza kati ya Machi 1 na Novemba 16 2020.

Wawili hao, hakimu alisema, walikamatwa baada ya kashfa hiyo ya watoto kupeperushwa na kituo cha utangazaji cha BBC.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka nimefikia uamuzi kesi dhidi ya Leparan na Awuor imethibitishwa,” alisema Bi Kimilu katika uamuzi wake. Bi Selina Awuor aliyekuwa anasimamia idara hiyo ya huduma za jamii hakujua wakati ule watoto hao waliruhusiwa kupelekwa kwa afisa watoto.

Badala ya kupelekwa kwa afisi hiyo watoto hao walipelekwa kwa gari iliyokuwa na wanunuzi na kutoroshwa.
Wakili Danstan Omari anayewatetea Leparan na Awuor aliomba ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia iwasilishwe kortini kabla ya adhabu kupitishwa.

Wawili hao watahukumiwa Septemba 26,2023.

  • Tags

You can share this post!

Uchumba kati ya magenge, wanasiasa na serikali...

Wakulima walia matapeli wawauzia mchanga na chokaa wakidai...

T L