• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Imani za uchawi kizingiti katika kukabili saratani

Imani za uchawi kizingiti katika kukabili saratani

IDARA ya afya katika Kaunti ya Kilifi imeeleza hofu kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wa kansa huenda hufa kwa sababu ya madai ya uchawi katika jamii nyingi za eneo hilo.

Kulingana na wahudumu wa afya, wagonjwa wengi huchelewa kutafuta matibabu hospitalini na imebainika kuwa wengi wao hutafuta mawaidha ya kitamaduni kwa vile huwa wanaamini wamerogwa.

Ili kukabiliana na tatizo hili ambalo limedumu kwa miaka mingi, idara ya afya katika kaunti sasa imeanzisha mikakati ya kutunga sheria ambayo itawahusisha wahudumu wa afya wa nyanjani moja moja katika kuhamasisha jamii kuhusu saratani.

Wahudumu hao wa nyanjani watatilia maanani saratani ya mlango wa uzazi ambayo kwa sasa ni tishio kwa wanawake kuliko saratani ya matiti, ingawa inaweza kutibiwa iwapo itagunduliwa mapema.

Akizungumza na wanahabari katika hospitali kuu ya rufaa ya Kilifi, Mshirikishi wa masuala ya afya ya uzazi kwa vijana, Bw Kennethe Miriti, alisema wanapanga kupambana vilivyo na dhana hiyo ya uchawi katika jamii na kuwataka wagonjwa kufika hospitalini wakati unaofaa ili kupata matibabu.

“Dhana potovu ya uchawi imekuwa changamoto kuu kwa kuwa mgonjwa hupatikana na saratani ila anaamini kuwa amerogwa na kurudi nyumbani kuenda kwa waganga na waombaji wa kidini,” akasema.

Kulingana na Bw Miriti, wagonjwa hao wa saratani hupoteza muda kwa waganga na waombaji na hutafuta matibabu hospitali baada ya kuugua kwa muda mrefu na wengi wao huwa katika hali mahututi.

Alisema sheria hiyo itahitaji idara ya afya kuwalipa wahudumu wa nyanjani ili kuwapa motisha ya kuendelea kujitotolea kufanya hamasa kwa jamii huko mashinani.

Kulingana na Bw Miriti, wahudumu wa afya watakapokuwa wakifanya kazi zao nyumba kwa nyumba, watawaelimisha familia hizo kuhusu ugonjwa wa saratani, dalili zake na pia umuhimu wa kuenda hospitalini kupata matibabu kwa wakati unaofaa.

“Hatua ya kuhusisha jamii imekuwa msaada kubwa na imetusaidia kutatua changamoto nyingi katika kaunti yetu ikiwemo mimba za mapema na pia tatizo la wanaume kutaka wanawake wapate idhini kwao kabla kupanga uzazi,”akasema.

Mbali na sheria hiyo, idara ya afya pia imetenga sehemu za kushughulikia ugonjwa wa saratani katika hospitali, kuweka vifaa katika vyumba vya saratani kupitia ufadhili wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kuwapa mafunzo maafisa wa afya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa.

Mshirikishi wa chanjo katika Kaunti ya Kilifi, Bi Christine Mataza, ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kupimwa iwapo wameambukizwa virusi vya HPV ambavyo husababisha saratani.

Pia wazazi wamehimizwa kuwapeleka watoto wao wa kike wa miaka 10 hadi 14 kupata chanjo dhidi ya virusi hivyo ili kuzuia saratani ya mlango wa uzazi.

Kaunti ya Kilifi inalenga kuwapa chanjo ya HPV wasichana 103,187.

  • Tags

You can share this post!

Wito waziri Machogu aruhusu wanafunzi kupata muda mwingi wa...

Nassir aendelea kubanwa kuhusu mawaziri wake

T L