• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Itumbi alia korti kumzuia kuhusisha mlalamishi na UDA

Itumbi alia korti kumzuia kuhusisha mlalamishi na UDA

Na JOSEPH WANGUI

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Dijitali katika Ikulu, Dennis Itumbi, anataka mahakama iondoe agizo la kumzuia kuhusisha mfanyabiashara wa Nairobi, Mike Maina Kamau na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto.

Kwenye ombi lililoidhinishwa kuwa la dharura na Jaji wa Mahakama Kuu, Jaden Thuranira, Bw Itumbi anasema kwamba kesi ya kuharibu jina iliyowasilishwa na mfanyabiashara huyo inanuiwa kutimiza malengo ya kisiasa.

“Sijawaahi kuchapisha habari za kumharibia jina Bw Kamau au mtu yeyote katika maisha yangu. Ninaheshimu sana kila mtu kama ninavyojiheshimu mimi binafsi,” akasema Bw Itumbi kwenye ombi alilowasilisha jana.

Kupitia wakili Kamotho Njenga, Bw Itumbi alisema agizo lililotolewa Septemba 24, 2021, halikutolewa kwa njia inayofaa.

Anadai Mahakama Kuu haina mamlaka ya kushughulika na kesi ya kuchafuliwa jina iliyowasilishwa na Bw Kamau, mmiliki wa Hoteli ya Marble Arch, Nairobi.

Wakili huyo alisema kesi hiyo inafaa kutupiliwa mbali kwa sababu ilipaswa kuwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu kulingana na sehemu ya 11 ya kesi za kijamii.

Anasema sheria inasema kesi kama hiyo inafaa kuwasilishwa katika korti ya chini zaidi iliyo na uwezo wa kuishughulikia.

Kulingana na Bw Itumbi, kesi ya Bw Kamau inapaswa kutupwa kwa kuwasilishwa katika mahakama isiyofaa. Anadai hakupewa nafasi ya kujitetea kabla ya agizo la kumzuia kuhusisha mfanyabiashara huyo na UDA.

“Agizo lililotolewa kufuatia malalamishi ya Bw Kamau ni unyanyasaji kwa Bw Itumbi ambaye hakupewa nafasi ya kusikilizwa kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa dhidi yake,” alisema wakili Kamotho.

Anasema kwamba kesi hiyo inanuiwa kuingilia uhuru wake wa kujieleza. Agizo hilo lilimzuia Bw Itumbi kuchapisha habari kumhusu Bw Kamau kwa siku 30.

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Mnyanyaso wa ngono kazini ukabiliwe

UFISADI: Wazito sasa wafinywa