• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kamati ya bunge lawamani kuhusu mzozo wa ardhi

Kamati ya bunge lawamani kuhusu mzozo wa ardhi

Na LUCY MKANYIKA

WAMILIKI wa ranchi ya Ndara B katika Kaunti ya Taita Taveta, wamekashifu Bunge la Kitaifa kwa kuchochea mzozo wa ardhi baina yao na maskwota katika shamba hilo.

Wakiongea mjini Voi, wamiliki hao walidai kuwa Kamati ya Ardhi ya Bunge la Kitaifa imezuia renchi hiyo kupata stakabadhi za ardhi ili kuanzisha Chuo Kikuu cha Diaspora katika eneo hilo.

Ujenzi wa chuo hicho umeleta utata baada ya baadhi ya wanaoishi katika ranchi hiyo kupinga mradi huo.

Kamati hiyo ya bunge ilizuru eneo hilo baada ya wenyeji hao kutuma maombi bungeni isaidie kutatua mzozo huo.

Akiongea na wanahabari Jumatatu, mwakilishi wa shamba hilo, Bw Ronald Mwang’ombe alisema kuwa mchakato wa kupata stakabadhi za kuhamisha ekari 1,500 za ranchi hiyo ili kujenga chuo hicho umekwama.

“Kila tukienda kwa afisi za ardhi tunaelezwa kuwa lazima tungoje ripoti ya bunge ndio tujue hatma yetu,” akasema.

Bw Mwang’ombe alisema kuwa walishangazwa na hatua hiyo na kuitaja kama mbinu ya kuhujumu haki zao.

Ranchi hiyo iliafikiana na wawekezaji Wakenya wanaoishi ng’ambo kuanzisha miradi tofauti katika ardhi hiyo.

Miradi hiyo inanuia kuunda nafasi 2,000 za kazi.

  • Tags

You can share this post!

OCPD apumzishwa kwa heshima zote

Polisi 4 wana kesi ya kujibu kwa mauaji ya wakili Kimani