• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 6:26 PM
Kaparo atawazwa msemaji wa jamii yake Laikipia

Kaparo atawazwa msemaji wa jamii yake Laikipia

Na JAMES MURIMI

WAZEE wa Kaunti ya Laikipia, Jumapili walimtawaza aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Francis Ole Kaparo kuwa Msemaji wa jamii ya Maasai katika gatuzi hilo.

Koo za Ilmumonyot, Lewaso, Ilng’wesi, Ilmokoodo na Ildigiri zilimtawaza Bw Kaparo kwenye hafla iliyoandaliwa nyumbani kwake Kimanjo, eneobunge la Laikipia Kaskazini.

Bw Kaparo ambaye hapo awali alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwiano na Utangamano (NCIC), pia aliwahi kuhudumu kama mbunge wa eneo hilo.

“Bw Kaparo alikuwa Mmaasai wa kwanza kufuzu na shahada ya sheria kutoka eneo hili, alihudumu kama mbunge hapa, akawa spika wa Bunge la Kitaifa kwa mihula mitatu na pia akahudumu kama mwenyekiti wa NCIC. Tumemteua kutokana na tajriba yake ya uongozi,” akasema Mzee aliyetambuliwa kwa jina Kinyaga.

Wazee hao pia walimwonya Seneta wa Narok Ledama Ole Kina dhidi ya kuzungumzia masuala yanayohusu kaunti hiyo na badala yake amakinikie siasa za kaunti yake ya Narok.

Pia walimwonya aliyekuwa mbunge wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel akome kuzungumza kwa niaba ya jamii hiyo kwa kuwa Bw Kaparo sasa yupo kwenye usukani.

Mbunge wa eneo hilo Sarah Lekorere alisema kwamba Mabw Ole Kina na Lempurkel ni kati ya wanasiasa ambao wamechangia utovu wa usalama katika eneo la Laikipia kutokana na matamshi aliyodai ni ya uchochezi.

Bi Lekorere alisisitizia kwamba jamii ya Wamaasai inafaa kutupilia mbali mila ya ukeketaji wa mabinti na wizi wa mifugo kwani zimepitwa na wakati mbali na kwamba zinarudisha eneo hilo nyuma kimaendeleo.

You can share this post!

DIMBA NYANJANI: Huyu ‘Mbappe’ wa Young Bulls atisha...

Njaa: UN yaahidi Sh13b kusaidia waathiriwa