• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
DIMBA NYANJANI: Huyu ‘Mbappe’ wa Young Bulls atisha Ligi ya Kitaifa

DIMBA NYANJANI: Huyu ‘Mbappe’ wa Young Bulls atisha Ligi ya Kitaifa

Na CHARLES ONGADI

WAKATI Ligi ya Kitaifa Daraja la Kwanza ikiwa pua na mdomo kutamatika kuna huyu straika chipukizi anayegonga vichwa vya habari kwa ustadi wake wa kupachika mabao.

Alex Kazungu Mwalimu, 19, maarufu kama ‘Mbappe’ wa timu ya Young Bulls FC ya Malindi, Kaunti ya Kilifi amedhihirisha kuwa moto wa kuotea mbali kwa ufungaji wa mabao.

Licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika ligi hii yenye ushindani mkali, chipukizi huyu yuko kifua mbele kwa ufungaji mabao akiwa na jumla ya mabao 21.

“Ndoto yangu ni kucheza katika ligi kuu na timu ya taifa kabla ya kuyoyomea ughaibuni kusaka lishe poa,” asema kwa makeke straika huyu jembe.

Wakati Young Bulls ilipokutana kwa mara ya kwanza na Gor Mahia Youth jijini Nairobi, benchi ya kiufundi ya K’Ogalo ilivutiwa sana na uchezaji wake.

Katika pambano hili, ‘Mbappe’ aliwasumbua sana madifenda wa Gor Youth licha ya kupata ushindi wa 3-0 katika mtanage huu.

Katika pambano la marudio katika uga wa Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Shanzu, timu hizi mbili ziliagana sare ya 1-1 huku ‘Mbappe’ akipachika bao hilo la Young Bulls.

Afisa mmoja wa K’Ogalo ambaye hakutaka kutajwa jina, alikiri waziwazi kwamba ‘Mbappe’ ni kama lulu inayosakwa na wengi kutokana na thamani yake.

Aidha, ‘Mbappe’ kwa upande wake anafichua kiu yake ni kuisakatia Bandari FC ama Wazito FC ila anakiri endapo K’Ogalo itamfikia na mkataba mzuri atakubali.

‘Mbappe’ alianza kusakata kabumbu akiwa na umri wa miaka saba (7) pekee akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Matsangoni, Kilifi mwaka wa 2007.

Pindi alipojiunga na shule ya upili ya Katana Ngala, Kilifi mwaka wa 2014, Matsangoni FC iliyokuwa ikishiriki ligi ya FKF Pwani kaskazini ilimsajili.

‘Mbappe’ alifaulu kuisaidia Matsangoni FC kushinda ligi ya FKF Pwani kanda ya kaskazini lakini timu hiyo haikuweza kujimudu kufedha kushiriki Ligi ya Kitaifa Daraja la pili.

Lakini ‘Mbappe’ alisajiliwa na Shanzu United FC iliyokuwa katika ligi ya taifa Daraja la Pili ambapo aliisaidia timu hiyo kutamba kabla ya kunyakuliwa na Congo Boys FCmwaka 2019.

Baada ya kipindi kifupi tu alivunja uhusiano wake na Congo Boys na kurudi Malindi alikojiunga na Young Bulls.

‘Mbappe’ asema bidii mazoezini imekuwa ndio siri ya mafanikio yake katika soka huku akiwahimiza wenzake hasa jimo a Pwani kujituma kila mara mazoezini.

“Siri ya ubora wangu ni mazoezi makali. Huwa nahakikisha kila asubuhi na jioni nawatangulia wenzangu uwanjani ili kujifua kinyama,” asema shabiki huyu wa Chelsea ya Uingereza.

Anaongeza kusema kila siku anahakikisha amefanya mazoezi zaidi ya wenzake kwa kuanza mapema na kumaliza kuchelewa.

You can share this post!

DIMBA: Ramsdale ‘nyani’ mpya asiyecheka na mtu...

Kaparo atawazwa msemaji wa jamii yake Laikipia