• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:55 AM
Kashfa ya sukari yatibuka wakurugenzi wanne washtakiwa kwa ulaghai wa Sh79Milioni

Kashfa ya sukari yatibuka wakurugenzi wanne washtakiwa kwa ulaghai wa Sh79Milioni

Na RICHARD MUNGUTI

WAKURUGENZI wa makampuni yanayouza bidhaa za vyakula wameeleza korti jinsi stakabadhi za makampuni yao zilivyotumika kuwasilisha kesi ya Sh79million katika mahakama kuu Kisumu katika kashfa ya sukari.

Na wakati huo huo wamiliki wa biashara katika miji ya Thika, Kerugoya na Karatina walimweleza hakimu mkuu Roseline Onganyo nakala za maombi ya kuuziwa sukari na bidhaa nyinginezo (LPOs) na kampuni ya United Millers Limited (UML) zilitumika kama ushahidi katika kesi waliyoshtakiwa wakurugenzi wa kampuni ya B N Kotecha & Sons Limited na wakurugenzi wa UML.

Wakitoa ushahidi wamiliki wa biashara hizo Bi Mercy Githitu , Bi Susan Njeri Munene na Bi Ruth Wambui walisimulia jinsi meneja wa mauzo wa kampuni ya UML Henry Munywoki Kavita alivyotembelea maduka yao katika miji ya Thika , Kerugoya na Karatina na kupewa oda (LPO) ya kuwauzia sukari maelfu ya magunia.

Bi Githitu alisema alimwagiza Bw Kavita kampuni ya UML imuuzie magunia 3,000 ya sukari , makatoni 5,000 ya mafuta ya kupikia na bandoo 2,000 za unga wa mahindi mnamo Aprili 15 2015.

Bi Munene , mmiliki wa kampuni ya Kabui iliyoko mjini Kerugoya alimwagiza Bw Kavita kampuni ya UML imuuzie magunia 5,000 ya sukari, makatoni 2,000 ya sabuni na bandoo 2,000 za unga wa ngano.

Mercy Githitu (kushoto)…Picha/RICHARD MUNGUTI

Bi Wambui ambaye kampuni yao ni Wama General Merchants, alieleza mahakama alimwagiza Bw Kavita kampuni ya UML imwuzie magunia 8,000 ya sukari na bidhaa nyinginezo.

Bi Wambui alisema anasimamia kampuni hiyo pamoja na mumewe Charles Macharia Wanjau.Wameaona sasa kwa muda wa miaka 25.Bi Wambui alisema alijulishwa na maafisa wa polisi kwamba LPO ya magunia 8,000 ya sukari ilikuwa inatumika katika kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya kuu ya Kisumu.

Mashahidi hao watatu walisema hawakuuziwa sukari na UML na wameshangaa nakala za LPO zao zilitumika kama ushahidi kortini.Lakini walieleza korti walipoiuliza UML sababu ya kutowauzia sukari walifahamishwa kulikuwa na matatizo ya kupata sukari kutoka kwa kampuni iliyokuwa inaiuzia.

Bi Wambui na Bi Munene walieleza mahakama Bw Kavita aliwaeleza kampuni yao ya UML iliteuliwa na kampuni nyingine B N Kotecha & Sons Ltd kuwa ikiiuzia sukari katika eneo la Mlima Kenya.

Wakiongozwa kutoa ushahidi na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka la umma Bi Everlyne Onunga na Vivian Kambaga mashahidi hao pamoja na Mkurugenzi wa B N Kotecha & Sons Bw  Hemal Kishor Kotecha waliwatambua Bw Kavita anayeshtakiwa pamoja na wakurugenzi wa UML Sunil Narshi Shah, Kamal Punja Shah na Magnesh Kumar Verma kortini.

Mashahidi hawa walieleza kuwa washtakiwa hao ndio waliofanya biashara nao na hatimaye stakabadhi za kampuni zao kutumiwa kama ushahidi katika kesi iliyoshtakiwa mahakama kuu ya Kisumu.

Katika kesi hiyo ya Kisumu LPOs za makampuni ya Githitu, Kabui , Wama na makampuni ya Huruma Stores, Alysam Stores,Cumulus Services, Linco Stores , J B Ministores na Alkin Mini Price Shop.

Wakurugenzi hao wa UML wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama kulaghai B N Kotecha & Sons Limited Sh79,471,600  wakidai walipata hasara kotecha ilipokosa kuiuzia sukari iliyokuwa imeagizwa na wateja wake.

Akitoa ushahidi Bw Kotecha alisimulia jinsi alifanya mkataba na Sunil kuwa akiuzia kampuni yao  ya UML sukari.Kuzindua biashara baina yao Sunil alimwagiza Kotecha auzie UML magunia 25,000 ya sukari kwa bei ya Sh76,250,000.

Baadaye akapewa oda ya kuuzia UML magunia 35,000 kwa bei ya Sh101,500,000.Pesa hizo Sh 176,750,000 ziliwekwa katika akaunti ya B N Kotecha katika benki ya KCB.

Lakini Bw Kotecha alimweleza Bi Onganyo kwamba makampuni ya Nzoia na Muhoroni alipokuwa akinunua sukari yalikumbwa na matatizo ya utengenezaji sukari.

Mkurugenzi huyo alisema waliandamana na Sunil hadi kiwanda cha Nzoia na kuona jinsi malori yalikuwa yamerundikana mle yakisubiri kununua sukari.Katika kipindi hicho mahakama ilifahamishwa Sunil na UML walimshtaki Bw Kotecha.

Alirudisha pesa Sh124,106,000 alizokuwa hajauzia UML sukari.

Baadaye UML iliwasilisha kesi nyingine ikiomba ilipwe Sh79,000,000 na Kotecha.Uchunguzi uliofanywa na kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya KMPG iligudua UML ilikuwa imetegemea LPOs feki kudai malipo hayo.

Washtakiwa hao walikanusha mashtaka saba ya kula njama za kulaghai , kughushi LPOs na kutumia LPOs kudai malipo kutoka kwa Kotecha.Washtakiwa wako nje kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000 kila mmoja.

Kesi inaendelea kusikizwa.

  • Tags

You can share this post!

Maseneta wapitisha hoja ya ghadhabu dhidi ya mawaziri...

Itumbi yuko na kesi ya kujibu katika dai kulikuwa na njama...