• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 3:58 PM
Kaunti ya Bungoma ilipoteza Sh2.6Bilioni tangu 2013

Kaunti ya Bungoma ilipoteza Sh2.6Bilioni tangu 2013

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya kesi za ufisadi imefahamishwa zaidi ya Sh2.6bilioni zililipwa makampuni 23 kinyume cha sheria katika kaunti ya Migori tangu 2013 Gavana Okoth Obado alipochaguliwa.

Mchunguzi wa tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC Robert Cheruiyot Rono aliwasilisha ushahidi wa kina jinsi makampuni ya familia moja yalipewa kandarasi mbali mbali na kulipwa mabilioni.

Bw Rono alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambapo Gavana Okoth Obado na watoto wake wanne na familia ya Bw Jared Oluoch Kwaga wameshtakiwa kwa uporaji wa pesa za kaunti.

Kampuni 23 za Bw Kwaga zilimlipa Bw Obado na watoto wake Sh73milioni. Bw Rono alisema baadhi ya kampuni hizo ni  Doutech Technology , Janto Construction, Joyush Business , Dankey Press, Deltrack ICT Services, Dolphus Software, Atinus Services, Bofad & Smga Agencies Limited, Mactebac Contractors, Majay Investiments, Marowa Stores, Mbingo Enterprises, Migwish Enterprises na Misoft Limited.

Pesa zilizolipwa kampuni hizi ni kama ifuatavyo,  Doutech Sh156,953,999.70 kati ya Mei na Oktoba 13 2016, Janto Sh130,609,144.25 (kati ya April na June 15 2019), Dankey (Sh90,402,113.80, Deltrack Sh185,684,Dolphas Sh335,000,Atinus Sh222,819,987,  Bofad &Smga Agencies Sh18.2milioni na Dankey Sh5.8milioni..

Bw Robert Rono (kulia) akiongozwa kutoa ushahidi na wakili wa serikali Eva Kanyuira…Picha/ RICHARD MUNGUTI

Bw Rono alieleza korti kampuni hizi na Bw Obado zilikaidi sheria. Hakimu mkuu Bw Lawrence Mugambi alielezwa kampuni hizi zilihusishwa na familia ya Bw Kwaga ambaye ndugu yake alikuwa anasimamia kitengo cha maabara katika hospitali ya kaunti ya Migori.

Akitoa ushahidi , mchunguzi wa tume ya kupambana na ufisadi nchini,Bw Rono , alifichua jinsi mamilioni ya pesa yalilipwa kampuni hizi 23 kutoka kwa akaunti za kaunti hiyo.

Bw Rono alieleza mahakama uchunguzi wa kina uliofanyiwa kampuni hizi 23 ulipelekea ufichuzi kwamba mkewe Bw Kwaga , mkewe Bi Christine Akinyi Achola, Mama yake Oluoch , Bi Penina Auma, ndugu zake (kwaga) Joram Opala Otieno na Patroba Ochanda Otieno na shemeji yake (kwaga) Carolyne Anyango Ochola walikuwa wamiliki wa kampuni hizi zilizofyoza pesa za kaunti ya Migori.

Bw Rono alisimulia jinsi habari zilipokelewa katika afisi za EACC kisha wachunguzi wakamwandikia barua Katibu wa Kaunti ya Migori Bw Christopher Rusana mnamo Agosti 2017 wakiomba stakabadhi za malipo kwa kampuni zilizotoa huduma kaunti hiyo.

Alisema mnamo Agosti 23, 2017, yeye na maafisa wengine walifika katika afisi ya Bw Rusuna lakini “hawakumpata.” Alisema walimpata sekritari wake kisha wakajitambulisha wanatoka EACC na kueleza sababu ya kufika kwao katika afisi hiyo ya Bw Rusuna.

Bw Rono alisema waliitisha nakala za malipo kwa makampuni katika kaunti hiyo tangu 2013. “Hatukuweza kupewa nakala hizo hadi Septemba 1 2017 kwa vile Bw Rusuna alisema hati wanazotaka ni nyingi mno na hazingeweza kupatikana  kwa wakati mfupi,” Bw Rono alieleza mahakama.

Mahakama ilielezwa na Bw Rono ambaye ni shahidi wa kwanza kutoa ushahidi alisema Mabw Samuel Omunga na Eliud Obonyo waliwasilisha nakala za hati walizoitisha katika afisi za EACC Nairobi.

“Ukaguzi wa hati hizo ulibaini makampuni 23 yaliyohusishwa na Bw Kagwa yalihusika na ufyozaji wa pesa za kaunti ya Migori,” alisema Bw Rono. Bw Rono alisoma makampuni hayo moja baada ya nyingine jinsi zilivyolipwa mamilioni ya pesa.

Huku ushahidi wa Bw Rono ukitafsiriwa kwa lugha ya Dholuo kuwezesha Mama Penina kuelewa kinachoendelea alisema ushahidi upo mahakamani utakaothibitisha jinsi sheria ilivunjwa katika ulipaji wa kampuni hizo.

Mahakama ilifahamishwa Sh256,703,688 ziligawanywa na familia ya Obado na Bw Kagwa kupitia makampuni kadhaa aliposhinda uchaguzi wa Ugavana 2013. Akisumulia ushahidi uliowasilishwa mahakamani na naibu msaidizi wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ADPP) Peter Kiprop alisema ufisadi ulikita mizizi katika kaunti hiyo.

Bw Kiprop anayeongoza kesi hiyo pamoja na Bi Hellen Mutellah na Bi Eva Kanyuira alieleza mahakama “atathibitisha jinsi Bw Obado na watoto wake wanne Achola Dan Okoth, Susan Scarlet Akoth na Jerry Zachary Okoth walifyoza Sh73milioni.”

Mahakama ilifahamishwa Bw Obado alipokea zaidi ya Sh73milioni. Pesa hizi  hakimu alielezwa zililipwa na kampuni za Bw  Kagwa. Pesa hizi mahakama ilifahamishwa zilitumika kulipia watoto wa Gavana huyu karo waliokuwa wakisoma Scottland,Uingereza na  Australia.

Bw Kiprop alisema mashtaka yatawaita mashahidi 59 aliosema watathibitisha jinsi watoto wa Obado walifaidi kutokana na pesa zilizotoka katika kaunti hiyo. Pia korti ilielezwa Bw Obado alifaidi na zaidi ya Sh34milioni zilizotumika kununua nyumba katika mtaa wa kifahari wa Lavington Nairobi.

Nyumba hiyo ilinunuliwa kwa jina la Susan Scarlet Akoth. Mawakili Kioko Kilukumi , George Kithi na wengine waliwasilisha maombi ya kupinga ushahidi wa Bw Rono lakini mahakama ikafutilia mbali malalamishi yao na kumruhusu afisa huyo wa EACC aliyechunguza kesi hiyo kutoa ushahidi.

Wakati mmoja Bw Kithi anayemwakilisha Bw Kwaga alitisha kujiondoa katika kesi hiyo.Kesi itaendelea.

Wakili Kioko Kilukumi (kushoto) na George Kithi…Picha/ RICHARD MUNGUTI
  • Tags

You can share this post!

KSG Ogopa imepania kushiriki FKF-PL miaka 4 ijayo

Liverpool wakaanga Watford bila huruma

T L