• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
KDF wajengea Waboni shule ya bweni

KDF wajengea Waboni shule ya bweni

Na Kalume Kazungu

WANAJESHI wa Kenya (KDF) wanaoendeleza operesheni ya usalama kwenye msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu wamekabidhi shule ya kwanza ya msingi ya bweni kwa jamii ya Waboni wanaoishi eneo hilo.

Shule hiyo iliyo katika kijiji cha Mangai ni ya mseto na ina ukubwa wa kusajili karibu wanafunzi 400 kwa wakati mmoja.

Shule hiyo imekuwa ikijengwa na kikosi cha KDF kinachoshughulika na masuala ya ujenzi na miundomsingi tangu Juni mwaka huu.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi majengo hayo yaliyojumuisha madarasa manane na mabweni mawili, Kamanda Msimamizi wa Operesheni Amani Boni, Kanali Meshack Kishoyian aliwasihi wakazi wa jamii ya Boni kutumia nafasi hiyo kutia fora masomoni.

Wakati huo huo, Bw Kishoyian alikabidhi majengo mawili mengine ya wanafunzi kusomea kwenye shule ya Bodhei Junction ambayo pia iko ndani ya msitu wa Boni.

Jumla ya shule sita hupatikana ndani ya msitu huo ulioko Lamu Mashariki. Shule hizo hata hivyo zimekuwa zikihudumia wanafunzi wa chekechea hadi darasa la nne pekee ilhali wale wa madarasa ya juu wakilazimika kusafirishwa hadi shule ya msingi ya bweni ya Mokowe Arid Zone iliyoko Lamu Magharibi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mangai, Khamis Mwaleso alisema furaha yake ni kuona wanafunzi wakisoma na kumaliza masomo yao ya msingi wakiwa shule moja badala ya kuhamishwahamishwa kwenye shule za mbali kila wanapofikia madarasa ya juu.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Bodhei Junction, Mohamed Menya, alisema kuimarishwa kwa usalama na miundomsingi kwenye shule za msitu wa Boni kumewasukuma walimu wengi kuwa na ari ya kufunza kwenye shule hizo.

Kwa upande wake aidha, Mkurugenzi wa TSC kaunti ya Lamu, Riziki Daido alisema mipango tayari inaendelea katika ofisi yake kuona kwamba idadi ya walimu wanohudumu kwenye shule za msitu wa Boni inaongezwa.

You can share this post!

Mkenya azuiliwa Uhispania kwa kugeuka mla watu

Wito mashirika yashirikiane kueneza bayoteknolojia nchini