• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wito mashirika yashirikiane kueneza bayoteknolojia nchini

Wito mashirika yashirikiane kueneza bayoteknolojia nchini

Na WANGU KANURI

[email protected]

Kongamano la Mawasiliano ya Bayosayansi Afrika (ABBC2021) limerai washikadau kutoka mashirika ya umma na ya kibinafsi yaungane ili uwezo wa Kenya kupitia bayoteknolojia uimarike.

Kongamano hilo ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili, lilifanywa katika hoteli ya Nairobi Sports Club kwa siku tano. Washikadau waliwaomba wanasayansi, wakulima, wanahabari, maajenti kutoka serikali na wanaotengeneza sera za umma kushirikiana katika kueleza umma kuhusu bayosayansi.

Bw Kennedy Oyugi, mtaalamu wa uchumi wa kilimo alisisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuboresha mazao yao ya ukulima kupitia mabadiliko ya kijeni. Ili kuafikia hayo, alisema wakulima hao watahitaji teknolojia mahususi zitakazowafaa.

“Hatua ambazo wanasayansi wetu wamefanya zinaridhisha. Hata hivyo, ninawapa changamoto wanasayansi hao kujitahidi katika kueleza mambo pasi kutumia misamiati ya kiteknolojia,” akasema Bi Betty Maina, Waziri wa Viwanda.

Teknolojia hii ya kubadilisha jeni huwapa wanasayansi uwezo wa kubadili chembechembe za DNA za viumbe ili hali zao ziboreke. Hivi sasa utafiti wa kubadili jeni za mihogo unaendelea nchini Kenya. Mafanikio ya utafiti huu yalionekana miaka miwili iliyopita wakati Kenya iliidhinisha pamba ya bayoteknolojia (BT.)

Prof Darington Oyugi, mkurugenzi mkuu katika Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Viumbe aliwarai wakuu katika nchi za Afrika kuharakisha kanuni mahususi zinazoangazia mabadiliko ya kijeni ili Kenya iweze kuongoza nchi zingine.

Mratibu wa PBS barani Afrika, Bw John Komen, alisherehekea jinsi serikali za Afrika zimejitahidi katika kuhakikisha kuwa sera za ukulima zinaleta mabadiliko katika nchi hizo.

“Serikali hizi za Afrika zimesaidia nchi hizo kukua kiuchumi, huku nafasi za ajira zikiongezeka na uchumi wa kilimo kukua. Hii imesaidia uvumbuzi wa ukulima unaotumia bayoteknolojia kukumbatiwa,” akaeleza Bw Komen.

You can share this post!

KDF wajengea Waboni shule ya bweni

Serikali yaanza kujenga barabara ya lami kuinua hadhi ya...