• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Kijiji machifu huzuia wenyeji kujenga nyumba za kisasa

Kijiji machifu huzuia wenyeji kujenga nyumba za kisasa

Na KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa kijiji cha Manda-Maweni, Kaunti ya Lamu wameshangaza wengi kwa kuishi katika nyumba zilizojengwa kwa udongo, nyasi na makuti ilhali kijiji hicho kina wafanyabiashara wengi wanaouza bidhaa za ujenzi wa nyumba nadhifu za kisasa.

Kijiji hicho cha wakazi takriban 2,000 ambacho kimekuwepo tangu mwaka wa 1982, huvutia wajenzi kwa uchimbaji wa mawe na utengenezaji wa matofali, kokoto, na rasilimali nyingine zinazotumika kwa ujenzi wa majumba ya kifahari kwingine Lamu.

Unapoingia huko, utakutana na bidhaa tele za ujenzi zikiwa zimepangwa tayari kusafirishwa hadi sehemu nyingine za Lamu ili kung’arisha majengo ya sehemu hizo za mbali.

Kuna sehemu zilizotengwa kijijini kuwa machimbo au migodi. Cha kustaajabisha na kusikitisha ni kwamba kijiji cha Manda-Maweni hakina nyumba ya kudumu na ikiwa ipo ni chache ambazo zinamilikiwa na watumishi wa umma.

Kwa wenyeji wanaofanya kazi ya kuchimba na kuuza bidhaa za ujenzi, nyumba zao ni za udongo, nyasi au makuti na ambazo idadi kubwa ziko katika hatari ya kuanguka ilhali nyingine tayari zimeporomoka na kusalia mahame.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wachimba-mawe aliye pia kiongozi wa jamii katika kijiji hicho, Bw Benson Ojuok, alikiri kuwa idadi kubwa ya wakazi wa kijiji hicho wana uwezo wa kujijengea nyumba za kudumu lakini wanadai kuna amri ya serikali inayowazuia kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wachimba-Mawe kijijini Manda-Maweni, Benson Ojuok wakati wa mahojiano na Taifa Leo. Anasema machifu wamekuwa wakiwanyima uhuru wa kujijengea nyumba za kudumu na kuleta hujuma kwenye suala zima la ardhi na hatimiliki. Picha/ Kalume Kazungu

Kulingana naye, machifu na manaibu wao wametoa amri ya ajabu kwa wananchi kujenga nyumba hizo zilizo maarufu kama madogo-poromoko, na unapopatikana ukijenga nyumba ya mawe au ya aina yoyote ya kudumu unahangaishwa na hata mjengo wako kubomolewa.

Isistoshe, anaongeza kuwa nyumba hizo za muda zinapoanguka huwa hazifai kukarabatiwa wala kujengwa upya kivyovyote isipokuwa kama una amri ya chifu au naibu wake.

“Mimi nimeishi Manda-Maweni kwa zaidi ya miaka 20 sasa. Tumeamriwa kutojenga nyumba za kudumu hapa licha ya kuwa tumeishi kwa ardhi hizi kwa muda mrefu. Huwezi kujiamulia kukarabati au kujenga nyumba hapa endapo chifu au naibu wake hajapenda. Ukikaidi amri yao na kuendeleza ujenzi basi nyumba yako itaangushwa na wewe mwenyewe kujipata pabaya,” akasema Bw Ojuok.

Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alisema hajapokea malalamishi yoyote kutoka kwa wakazi hao kuhusiana na madai ya machifu kuingilia suala la ardhi zao.

“Chifu hana jukumu lolote katika suala zima la ardhi. Ninashangaa kwani sijapokea malalamishi yoyote kuhusiana na chifu au naibu wa chifu anayehangaisha wakazi kuhusiana na ardhi,” akasema.

Kulingana naye, habari alizo nazo ni kwamba kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya wakazi wa Manda-Maweni na mwekezaji wa kibinafsi anayedai wananchi hao wamekalia ardhi yake kinyume cha sheria.

Bw Macharia aidha aliahidi kuchunguza suala hilo na kuwataka wananchi kuwa watulivu.

Katibu wa Muungano wa Wachimba-mawe kijijini humo, Bw Jackson Mwiti ambaye ameishi pale kwa zaidi ya miaka 30 alisema wanakandamizwa dhidi ya kujiendeleza kimaisha ilhali rasilimali zao zinatumiwa kunadhifisha miji mingine ya Lamu.

Mbali na hayo, kuna baadhi ya wakazi ambao hata mabanda au nyumba hizo za muda hawana. Wakati mwingi wao hulazimika kulala mabarazani au ndani ya machimbo ya mawe kwani wamekatazwa kujenga.

Bw Mwiti aliiomba serikali ya kaunti ya Lamu na ile ya kitaifa kupitia Tume ya Ardhi nchini (NLC) kutekeleza usoroveya wa haraka wa ardhi kijijini Manda-Maweni na kuhakikisha wananchi wanapewa hatimiliki za ardhi ili wawe na uhuru wa kujiendeleza.

“Tumechoka kuchimba na kusafirisha rasilimali hizo nje ya kijiji chetu ilhali sisi wenyewe hatufaidi. Suluhu ya kipekee ni ardhi tunazokalia zifanyiwe usoroveya na kila mmoja wetu apewe kipande chake cha ardhi na hatimiliki kujiendeleza kivyake. Bila hivyo tutasalia kuitwa watu wa mtaa wa mabanda wa Manda-Maweni licha ya kwamba uwezo wa kujenga nyumba za kudumu tunao,”akasema Bw Mwiti.

Bi Charity Wangeci ambaye ni wa mpango wa Nyumba Kumi kijijini Manda-Maweni, anaitaka serikali kupitia idara ya ujasusi kuwachunguza machifu na manaibu wao kwa madai ya kuingilia masuala ya ardhi na hata kuwahangaisha wakazi eneo hilo kila kuchao.

Mama Charity Wangeci wa mpango wa Nyumba Kumi kijijini Manda-Maweni, akieleza vile machifu na manaibu wao walivyokuwa kizingiti cha wananchi wa Manda-Maweni kujiendeleza. Sasa anataka maafisa hao wa utawala kuchunguzwa. Picha/ Kalume Kazungu
  • Tags

You can share this post!

Raila, Joho wamwacha Nassir kwa tundu la simba

Kenya Simbas yararuliwa na Terenga Lions ya Senegal raga ya...