• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Kocha Allegri awataka Juventus wamsajili upya kiungo Paul Pogba kutoka Manchester United

Kocha Allegri awataka Juventus wamsajili upya kiungo Paul Pogba kutoka Manchester United

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Massimiliano Allegri amewataka waajiri wake Juventus kumsajili upya kiungo Paul Pogba wa Manchester United muhula huu.

Pogba ambaye ni raia wa Ufaransa, kwa sasa yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na Man-United wamemsajili kiungo mvamizi Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund.

Kwa mujibu wa gazeti la 90min nchini Italia, ujio wa Sancho utamweka Pogba katika ulazima wa kusugua benchi ikizingatiwa kwamba kocha Ole Gunnar Solskjaer atapendelea sana kumchezesha kwa pamoja na Bruno Fernandes nyuma ya wavamizi wakuu wa Man-United.

Pogba, 28, alihudumu kambini mwa Juventus kwa miaka minne baada ya kuondoka ugani Old Trafford mnamo 2012. Alinolewa na Allegri katika misimu yake miwili ya mwisho kambini mwa Juventus kabla ya kubanduka jijini Turin na kurejea Man-United kwa kima cha Sh12.4 bilioni mnamo 2016.

Licha ya Ufaransa kuondolewa mapema kwenye kampeni za Euro mwaka huu, mchango wa Pogba umehisika pakubwa kiasi cha kuchochea vinara wa Man-United kumzungumzia wakala wake Mino Raiola kuhusu uwezekano wa kurefusha mkataba wa kiungo huyo.

Ingawa hivyo, gazeti la 90min linashikilia wapo baadhi ya vinara wa Man-United wanaopinga hatua ya Pogba kupokezwa mkataba mpya utakaomshuhudia akiwa sogora anayedumishwa kwa mshahara mnono zaidi (Sh62.4 milioni kwa wiki) uwanjani Old Trafford.

Mbali na Juventus, kikosi kingine kinachowania maarifa ya Pogba ni Real Madrid ambao pia wanamfukuzia Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain (PSG).

Allegri alirejea kudhibiti mikoba ya Juventus mnamo Mei 2021 licha ya kikosi hicho kumpiga kalamu mnamo Mei 17, 2019. Kurejea kwake kulichochewa na haja ya kujazwa kwa pengo lililoachwa na Andrea Pirlo aliyepigwa kalamu.

Gazeti la 90min limeshikilia kuwa kurejea kwa Pogba kambini mwa Juventus huenda pia ukatumiwa na Man-United kufanikisha marejeo ya Cristiano Ronaldo uwanjani Old Trafford. Ronaldo ambaye ni raia wa Ureno ni mshindi mara tano wa taji la Ballon d’Or. Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid bado ni kipenzi cha mashabiki uwanjani Old Trafford licha ya kwamba atakuwa akifikisha umri wa miaka 37 mnamo Februari 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Man-United waambia kiungo Donny van de Beek kuwa yuko huru...

Balaa mikopo ya Kenya ikifika Sh9tr