• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Kocha Nuno Espirito pazuri zaidi kuwa mrithi wa Mourinho kambini mwa Spurs

Kocha Nuno Espirito pazuri zaidi kuwa mrithi wa Mourinho kambini mwa Spurs

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Wolves, Nuno Espirito Santo, yuko pazuri zaidi kutwaa mikoba ya ukufunzi kambini mwa Tottenham Hotspur.

Spurs waliomtimua mkufunzi Jose Mourinho mnamo Aprili 19, 2021 bado wanatafuta kocha mpya atakayewaongoza kuanzia msimu mpya wa 2021-22.

Spurs wanaanza kumhemea Espirito baada ya juhudi zao za kumwajiri kocha wa zamani wa AS Roma, Paulo Fonseca, kutibuka. Aidha, fununu za kuajiriwa kwa kiungo wa zamani wa Italia, Gennaro Gattuso aliyebanduka Fiorentina baada ya siku 23 pekee, zilikumbana na maandamano makali kutoka kwa mashabiki wa Spurs.

Espirito amekuwa akihusishwa na mikoba ya Everton pamoja na Crystal Palace tangu akatize rasmi uhusiano wake na Wolves mwishoni mwa msimu wa 2020-21.Mnamo Juni 21, 2021, mvamizi wa zamani wa Spurs, Jurgen Klinsmann alifichua kiu ya kupokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa kikosi hicho.

Hiyo ilikuwa baada ya jaribio la Spurs kumshawishi kocha wa Sevilla, Julen Lopetegui kujiunga nao kuambulia pakavu.Mapema Juni 2021, Spurs walikuwa wakihusishwa pakubwa na uwezekano wa kumwajiri aliyekuwa kocha wa Inter Milan, Antonio Conte, huku wakijaribu pia kumnyemelea upya mkufunzi wao wa zamani, Mauricio Pochettino ambaye kwa sasa ananoa Paris Saint-Germain (PSG).

Espirito, 47, aliondoka kambini mwa Wolves baada kuhudumu uwanjani Molineux kwa kipindi cha miaka minne. Akiwa huko, alishinda taji la Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) katika msimu wake wa kwanza kabla ya kuongoza Wolves kuambulia nafasi ya saba kwenye misimu miwili iliyofuata kwenye soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Wolves walikamata nafasi ya 13 kwenye msimamo wa jedwali la EPL mnamo 2020-21.Espirito ambaye ni raia wa Ureno, alitia saini mkataba mpya wa miaka mitatu kambini mwa Wolves mnamo Septemba 2020.

 

  • Tags

You can share this post!

Kanuni ya bao la ugenini yaondolewa kwenye soka ya bara...

Eti ni nadhifu, tupelekane wapi?’