• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Kongamano la siku tatu MKU lanogesha biashara Thika

Kongamano la siku tatu MKU lanogesha biashara Thika

NA LAWRENCE ONGARO

KONGAMANO la siku tatu linalojumuisha vyuo vikuu kadha vya bara Afrika lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) hivi majuzi mjini Thika. 

Kongamano hilo pia lilihusisha chuo cha Vincent Pol Of Lublin cha nchini Poland.

Wageni zaidi ya 100 walitoka vyuo mbalimbali kutoka bara la Afrika.

Baadhi ya vyuo hivyo ni Kyambogo (Uganda) Chukwuemeka Odumegwu Ojukwu (Nigeria), Makeni (Sierra Leone) na Chuo Kikuu cha Eldoret (Kenya). MKU ndio ilikuwa mwenyeji.

Maswala ya ubunifu na maswala ya uongozi pamoja na masuala ya kiuchumi yalijadiliwa kwa takriban siku tatu.

Wageni wote waliohudhuria kongamano hilo walikaa katika hoteli tofauti mjini Thika. Baadhi ya hoteli hizo ni Paleo, Maxland, St Luke Cravers,  na Eton.

Dkt Henry Yatich aliye msimamizi mkuu wa kitengo cha utafiti MKU, ndiye aliyeteuliwa kama mwenyekiti wa kongamano hilo.

Hafla hiyo pia ilileta pamoja washika dau wa umma na kutoka sekta ya kibinafsi ili kujadili kuhusu usalama na maswala ya uchumi.

“Hafla hii ni ya kipekee kufanyika na kujumuisha vyuo tofauti tangu kushuhudiwa janga la Covid-19,” alisema Dkt Yatich.

Chansela wa MKU Prof Deograttus Jaganyi alisema mbali na kufuatilia na kuhudhuria moja kwa moja katika ukumbi wa Mwai Kibaki Convention Centre, washiriki wengine walifuatilia kupitia mtandao.

Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kilikuwa mwenyeji wa kongamano muhimu wiki hii ya Pasaka ambapo maswala ya ubunifu na maswala ya uongozi pamoja na masuala ya kiuchumi yalijadiliwa kwa takriban siku tatu. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alisema wamekuwa na ushirikiano mzuri kati ya chuo cha Vincent Pol cha Poland na MKU.

Alisema tayari wameweka mipango ya kujiendeleza kupitia mpango wa elimu almaarufu Erasmus Programme.

Dkt Yatich alivipongeza vyuo vyote vilivyohudhuria hafla hiyo na kupendekeza kila mara wawe wakipanga hafla nyingi ili kujumuisha wasomi na washika dau wengine pamoja.

Dkt Vincent Gaitho ambaye ni Pro-chansela wa MKU, alisema kongamano hilo ni muhimu kwa sababu linapatanisha wasomi tofauti ambao wanachangia maswala mengi katika ulimwengu.

Dkt Jane Nyutu ambaye ni mwanzilishi wa  chuo cha MKU kwa niaba ya wakuu wa bodi ya chuo hicho alipongeza wageni wote waliohudhuria hafla hiyo.

“Tutaendelea kushirikiana na vyuo tofauti ili kuendeleza masomo katika kiwango cha juu,” alisema Dkt Nyutu.

Dkt Dick Andala ambaye alikuwa mgeni kutoka idara ya utafiti ya Kenya National Research Fund (KNRF) alisema kuna wasomi wachache ambao wanaendeleza uzamifu katika chuo cha MKU kwa ada ya Sh129 milioni.

  • Tags

You can share this post!

Gavana alia wizi wa maji 001

‘Msinisulubishe kwa mara ya pili’

T L