• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kuhalalisha au kutohalisha bangi kutahitaji sera mwafaka

Kuhalalisha au kutohalisha bangi kutahitaji sera mwafaka

Na MARY WANGARI

[email protected]

KWA muda sasa, mjadala mkali umekuwa ukitokota kuhusu kuhalalisha au kutohalalisha bangi humu nchini kiasi cha kesi kuwasilishwa kortini kuhusiana na suala hilo linalozingirwa na utata.

Katika kisa cha hivi majuzi, Kundi la Wafuasi wa Dini ya Rastafari (RSK) liliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu, likitaka matumizi ya bangi manyumbani kwao na maabadini yahalalishwe, jambo ambalo kwa sasa ni marufuku.Katika mkondo ambao wengi hawakutarajia, Rais wa Muungano wa Wanasheria Nchini (LSK) Nelson Havi aliahidi kuhalalisha matumizi ya bangi aliyotaja kama ‘mmea mtakatifu’ akihoji kuwa bangi ina manufaa kiafya kwa wananchi.

Bosi huyo wa LSK alisema hayo kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, alipoungana na viongozi na Wakenya Jumapili, kuadhimisha Siku ya Mazingira.Bangi inasheheni manufaa chungunzima kijamii na kitamaduni hasa ikiwa matumizi yake yanaweza kudhibitiwa kupitia sera madhubuti na vilevile kujumuishwa katika sheria zinazodhibiti dawa nchini.

Aghalabu, bangi hutumiwa kama tiba ya kiasili, katika starehe za burudani na kuwachangamsha watu wanaofanya kazi hasa za sulubu zinazohitaji matumizi ya nguvu nyingi.Hata hivyo, mjadala kuhusu uhalalishaji wa bangi au la umezingirwa na utata mwingi kwa muda mrefu kutokana na kukosa uelewa, kasumba potovu, kuingiza hisia na data zilizopitwa na wakati kuhusiana na matumizi ya bangi nchini.

Ndiposa umuhimu wa mazungumzo jumuishi yatakayowezesha kubuni sera thabiti kuhusu matumizi ya mmea wa bangi pasipo kuegemea au kuumiza upande wowote, hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.Bangi ni miongoni mwa vileo vinavyotumika kwenye starehe za burudani ikiwemo uvutaji shisha ambao ulikwisha pigwa marufuku, unywaji pombe na uvutaji tumbaku.

Ni sharti serikali ifanyie marekebisho Sheria kuhusu Matumizi ya Vileo 1992 pamoja na kufadhili utafiti wa kina kuhusu manufaa na madhara ya matumizi ya bangi kwa mtu binafsi na kwa ujumla, ili kupata mwelekeo thabiti.Isitoshe, ikizingatiwa kuwa bangi imeendelea kutumiwa tangu jadi licha ya sheria zinazopiga marufuku matumizi yake, ni bayana kuwa ni muhimu kushirikisha umma katika mazungumzo ya kina katika juhudi za kupata suluhisho la kudumu.

Lengo hasa ni kudhibiti matumizi ya bangi kwa kuijumuisha katika sera kuhusu matumizi ya dawa nchini kutokana na manufaa yake kiafya, hasa ikizingatiwa kwamba tayari kuna sheria inayotoa mwongozo kuhusu tiba za kiasili.Ni dhahiri kuwa hatuwezi kupuuza vitendo vya uhalifu vinavyotokana na matumizi mabaya ya bangi ikiwemo dhana hasi inayozingira mmea huo unaoainishwa kama mojawapo wa mihadarati.

Kuwepo kwa sera na sheria kabambe hata hivyo, kuhusu matumizi ya bangi, mazingira inamofaa kutumiwa sawia na mihadarati mingine kama vile sigara na pombe, kutasaidia pakubwa kuondoa mivutano ya kila [email protected]

  • Tags

You can share this post!

Achani arai wanawake wajitokeze zaidi kisiasa

ODM yaomboleza