• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mabingwa warejea!

Mabingwa warejea!

KAMBI ya Kenya Lionesses imejaa furaha inapolenga kushiriki Kombe la Afrika la mpira wa vikapu la kinadada (AfroBasket) mwezi Septemba baada ya kuvua Misri ubingwa wa Zoni ya Tano mnamo Jumapili.

Ilichabanga miamba hao 99-83 katika fainali ya Zoni ya Tano iliyosisimua jijini Kigali, Rwanda.Ingawa Lionesses wamekiri kuwa kibarua kigumu kinawasubiri nchini Cameroon, kila mzungumzaji katika timu hiyo iliporejea nchini mnamo Jumapili usiku, hakuficha raha waliyopata kwa kulipiza kisasi dhidi ya Misri ambayo imewasumbua miaka nyingi.

“Kupiga Misri ni kitu tumekuwa tukisubiri kwa hamu na tuna furaha sana tulifaulu katika fainali,” alisema nyota Felmas Koronga ambaye alifunga alama 24 katika fainali. Alitazwa mshambuliaji bora kwenye mashindano hayo wa pembeni kushoto.

Mzawa wa Amerika, Victoria Reynolds, ambaye babake Bernard Wanjara alichezea Kenya kwenye Kombe la Afrika mwaka 1993, aliibuka mfungaji bora katika fainali akiwa na alama 25. Reynolds aliyeshinda tuzo ya mshambuliaji bora wa pembeni kulia na mchezaji bora kwenye mashindano hayo yaliyovutia mataifa manne – Kenya, Misri, Rwanda na Sudan Kusini – aliapa kuwa watafanyia Kenya kazi nzuri jijini Yaounde.

Mchezaji mbunifu Natalie Akinyi, ambaye alipachika alama 12 katika fainali pamoja na kusuka pasi kadhaa muhimu zilizofungwa, alikiri kuwa dimba la AfroBasket litakuwa ngumu, “lakini tutajitolea kwa dhati kutafuta matokeo mazuri”.

Lionesses ya kocha George Mayienga ilikutana na Waziri wa Michezo Amina Mohamed katika hoteli moja mtaani Nairobi West baada ya kuwasili. Aliipongeza kwa kazi nzuri na kuahidi itapata usaidizi kikamilifu kabla ya AfroBasket.

Alisema hayo wakati wa dhifa ya usiku iliyohudhuriwa na maafisa kutoka Shirikisho la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) akiwemo mwenyekiti Paul Otula, afisa kutoka Baraza la Michezo nchini Kenya (KNSC) Charles Nyaberi na Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF) Moses Mbuthia, miongoni mwa wengine.

Aidha, Mayienga aliambia Taifa Leo kuwa wasiwasi, makosa kadha mechini na kutochunguza vyema wapinzani wake kulisababisha Lonesses ichapwe na Rwanda na Misri katika mechi za makundi.Hata hivyo, alifurahia kuwa timu hiyo ilijinyanyua na kulipiza kisasi ikinyakua tiketi moja iliyokuwa mezani.

Mbali na Lionesses, timu nyingine zilizojikatia tiketi ya AfroBasket ni Nigeria, Senegal, Mali na Msumbiji wote waliofika nusu-fainali ya 2019, wenyeji Cameroon na washindi wa Zoni ya Pili Cape Verde.

  • Tags

You can share this post!

Je tutajifunza lini?

CF Montreal anayochezea Wanyama yang’ata Cincinnati...