• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Madereva, wamiliki wa tuk-tuk waandamana Mombasa kwa kuhangaishwa na maafisa wa kaunti

Madereva, wamiliki wa tuk-tuk waandamana Mombasa kwa kuhangaishwa na maafisa wa kaunti

Na SIAGO CECE

WAHUDUMU wa tuk-tuk mjini Mombasa waliziba barabara kadhaa mjini huku wakifanya maandamano kulalamikia kuhangaishwa na maafisa wa kaunti.

Maandamano hayo yalifanyika wakati serikali ya Kaunti ya Mombasa imekuwa ikitekeleza sera ambazo inasema zinalenga kuhakikisha hakuna wahalifu wanaojificha miongoni mwa wahudumu hao.

Wakati wa maandamano yao, walilalamika kuhusu sera mpya ya kaunti iliyowahitaji kulipa Sh1,000 ili wapewe kibandiko maalum cha usalama.

Baadhi ya wahudumu wa tuk-tuk waandamana mjini Mombasa, Juni 14, 2021. Picha/ Kevin Odit

Bw Joseph Karisa, mmoja wa waandamanaji hao alidai kuwa hatua za kaunti zinavuruga biashara yao hata baada ya kulipishwa ada ya Sh1,200 kila mwezi ya kuegesha tuk-tuk mjini.

Ada mpya ya Sh1,000 inapaswa kulipwa kufikia Jumanne, Juni 15, 2020 pamoja na ada ya maegesho.

Wahudumu hao pia walilalamika kuwa ada mpya ni ya juu sana kwani bei ya mafuta imeongezeka na nchi inakabiliwa na nyakati ngumu za kiuchumi.

Hapo awali, serikali ya kaunti ilisema hatua imenuia kukomesha uhalifu unaofanywa na baadhi ya wahudumu wa tuk tuk katika kaunti hiyo.

Kaunti hiyo ilisema mpango wa kupeana vibandiko kwa kila tuk-tuk itahakikisha kaunti ina maelezo yote kuhusu wahudumu halali ili iwe rahisi kuwatafuta endapo tuk-tuk zao zitahusika katika visa vya uhalifu.

You can share this post!

Dhuluma: Mbunge ahimiza wanawake wazungumze waziwazi badala...

Nasa sinaswi tena