• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 6:26 PM
Madiwani wataka ushuru wa muguka uongezwe ili kuokoa ndoa

Madiwani wataka ushuru wa muguka uongezwe ili kuokoa ndoa

Na ALEX KALAMA

DIWANI wa wadi ya Garashi iliyo katika Kaunti ya Kilifi, Bw Peter Ziro amewasilisha hoja ya kutaka ushuru wa muguka uongezwe katika kaunti hiyo.

Kulingana na diwani huyo, wanawake wengi walio kwenye ndoa wamekuwa wakilalamika kukosa kufurahia tendo la ndoa na waume zao kutokana na wanaume hao kutumia muda mwingi kutafuna muguka mchana na usiku.

Bw Ziro amedai kuwa bei rahisi ya muguka ni chanzo cha wakazi wengi kujitosa katika uraibu wa kutafuna majani hayo mabichi.

“Nimepokea malalamishi mengi kwamba waume hutumia muda mwingi kutafuna muguka. Kwa hivyo itakuwa vyema tukiongeza ushuru ili wengi washindwe kununua ili tunusuru hizi ndoa,” alisema Bw Ziro.

Juhudi nyingi za awali katika baadhi ya kaunti kitaifa kupiga marufuku biashara ya muguka huwa zimegonga mwamba kwa sababu zisizojulikana wazi.

Aidha Bw Ziro aliongeza kuwa wahudumu wengi wa bodaboda hukosa nidhamu pindi wanapotafuna muguka.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Diwani wa Malindi Mjini, Bw David Kadenge ambaye alisistiza kuwa endapo bunge la kaunti ya Kilifi litakosa kupitisha hiyo, basi atalazimika kupeleka hoja nyingine ya kupiga marufuku muguka Kaunti ya Kilifi.

“Naunga mkono mswada huo ambao tunatarajia kuujadili bungeni wiki ijayo, ili tukabiliane na matatizo ambayo yanatokana na uraibu huu,” akasema Bw Kadenge.

Hayo yanajiri siku chache tu baada ya mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu mjini Malindi Famau Mohammed Famau kutoa wito kwa bunge la kaunti ya Kilifi na mabunge ya pwani kupitisha miswada ya kupiga marufuku utumizi wa muguka.

You can share this post!

Demu avamia polo kwa kutomtongoza

Nafasi ya Oimeke katika EPRA yajazwa