• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mahakama yaruhusu Wakenya wale mahindi GMO

Mahakama yaruhusu Wakenya wale mahindi GMO

Na RICHARD MUNGUTI

WAKENYA sasa wanaweza kuanza kula mahindi yaliyokuzwa kisayansi baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kutupilia mbali kesi ya kupinga uamuzi wa serikali wa kuagiza na kulima mazao hayo maarufu kama GMO.

Jaji Oscar Angote alitupilia mbali kesi hiyo, akisema kuwa nchi imeweka mfumo thabiti wa udhibiti wa usalama ambao lazima uzingatiwe kabla ya matumizi ya GMO.

Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK) kilikuwa kimepinga kuondolewa kwa marufuku hiyo, hatua iliyochukuliwa na Baraza la Mawaziri mnamo Oktoba 3, mwaka jana.

Marufuku hiyo ilikuwa imedumu kwa miaka kumi.

Baraza la Mawaziri lilisema kuondolewa kwa marufuku hiyo kulinuiwa kukabiliana na uhaba wa chakula kufuatia ukame mbaya zaidi kukumba eneo la Upembe wa Afrika katika miaka 40.

Chama cha Wanasheria cha Kenya, kilipinga kikisema uamuzi huo haukuwa wa kikatiba kwani kulikuwa na wasiwasi juu ya usalama wa mazao hayo.

Lakini Jaji Angote aliamua kwamba hakukuwa na ushahidi wa kuonyesha madhara yoyote kwa afya ya binadamu kutokana na ulaji wa chakula cha GMO.

Alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha kwamba asasi za serikali zimekaidi sheria na mwongozo kuhusu vyakula vilivyokuzwa kisayansi.

Kuhusu kilimo cha vyakula vya GMO, Jaji Angote, alisema hakuna ushahidi aliopewa kuzingatia akifanya uamuzi kuhusu athari zilizotarajiwa katika ukuzaji wa vyakula hivi.

Jaji huyo alisema, uuzaji wa vyakula hivi ng’ambo haswa mahindi unatazamiwa kuimarisha uchumi.

“Kama nchi, tunahitaji kuamini taasisi tulizonazo na kuzikosoa zinapokiuka sheria pekee,” Jaji Angote alisema, akirejelea mashirika ya serikali ambayo yanadhibiti vyakula vya GMO.

Kenya, kama mataifa mengine mengi ya Kiafrika, ilipiga marufuku mazao ya GMO kutokana na masuala ya afya na usalama na kulinda mashamba ya wakulima wadogo walio wengi nchini.

Wanaharakati pia walipinga kuondolewa kwa marufuku hiyo, wakisema kuwa ilifungua soko kwa wakulima wa Amerika kuuza mazao yaliyokuzwa kisayansi nchini na kutishia maisha ya wakulima wadogo.

Hata hivyo, wanasayansi walisisitiza kuwa kilimo cha mazao yanayokuzwa kisayansi ni salama kutumika kama chakula.

Pia walisema, chakula cha mimea iliyokuzwa kisayansi kina virutubisho sawia na vyakula vinginevyo.Wanasayansi zaidi ya 90 kutoka Mtandao wa Vyuo vya Sayansi Afrika (NASAC), wametoa wito kwa mataifa ya Afrika kukubali teknolojia ya kisasa ya ukuzaji mimea ili kuboresha mazao ya kilimo.

Wakiongozwa na Rais wa NASAC, Profesa Nobert Hounkonnou, na Profesa Ratemo Michieka, katibu mkuu wa NASAC, walisema kuwa nchi na bara lote limegubikwa na midahalo kuhusu vyakula vya GMO.

Uamuzi huo utafungua milango kwa serikali kuweka mikakati ya kuanzisha kilimo cha mazao hayo nchini au kuyaagiza kutoka mataifa ya nje kukabiliana na uhaba wa chakula.

  • Tags

You can share this post!

Pasta Ezekiel, mhubiri Mackenzie waitwa mbele ya kamati...

Whozu akiri hana kwake, ndio maana anaishi kwa mpenziwe...

T L