• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:26 PM
Mahangaiko tele, wakazi Juja Farm walazimika kukarabati barabara wenyewe

Mahangaiko tele, wakazi Juja Farm walazimika kukarabati barabara wenyewe

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa eneo la Juja House-Gicigo-ini, Juja Farm, Kaunti ya Kiambu, wameamua kukarabati barabara wenyewe baada ya kushindwa na hali ya kusafiri.

Licha ya hayo kuna daraja lililoko eneo hilo ambalo mvua ikinyesha huwa ni hatari kwa maisha yao.

Bi Jane Muthoni mkazi wa eneo hilo alidai kuwa mara nyingi wao hufanya ujima kujaza mawe kwenye barabara hiyo ili iweze kupitika.

“Wakati mwingi tunafanya kazi ya ziada kama wakazi wa eneo hili kuona ya kwamba tunajishughulikia kutengeneza sehemu ya kupitia. Hata wakati mwingine tunatafuta trekta ya kuchimba eneo hilo,” alisema Bi Muthoni.

Bw John Kimani ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo anasema watalazimika kama wakazi wa huko kufanya ‘harambee’ kwa kuungana pamoja ili kuunda barabara hiyo.

Alisema wakati wa mvua kubwa biashara nyingi hukwama kwa sababu hakuna jinsi bidhaa zitavyoweza kupitia kutoka upande mmoja hadi mwingine.

“Sisi wakazi wa Juja Farm tungetaka Kaunti ya Kiambu angalau ifanye jambo kuona ya kwamba sisi kama wakazi wa eneo hili tunapata barabara nzuri itakayotufaa kwa mahitaji yetu ya kila mara,” alisema Bw Kimani.

Naye Bi Mary Njeri anasikitika kuwa mmoja wa jamaa wake alisombwa na maji mwaka 2020 wakati mto ulio karibu ulifurika na kusomba daraja wanalotumia kila siku.

“Tukio hilo huwa linanipa hofu nikikumbuka jinsi ambavyo daraja hilo ni legevu. Jambo la dharura linastahili kutendeka,” alifafanua Bi Njeri.

Mnamo Jumamosi, mwaniaji wa kiti cha ubunge cha Juja Dkt Joseph Gichui, aliungana na wakazi wa eneo hilo kurekebisha daraja hilo na kujaza mawe katika barabara hiyo mbovu.

“Wakazi wa eneo hilo wamekuwa na shida kubwa ya barabara mbovu na daraja lenye hatari. Kwa hivyo ni vyema kuwasaidia,” alisema Dkt Gichui.

Aliitaka Kaunti ya Kiambu ifanye hima kuona ya kwamba matakwa ya wakazi hao yanashughulikiwa mara moja.

Alihofia kuwa iwapo hatua ya haraka haitachukuliwa basi wakazi hao wa Juja Farm watapata shida ya kusafiri.

  • Tags

You can share this post!

Alexis Sanchez afunga mabao mawili na kusaidia mabingwa...

Mamelodi Sundowns anayochezea beki Brian Mandela...