• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Maji ya mafuriko Mto Ngong yatatiza usafiri kati ya mitaa ya Kayaba na Hazina

Maji ya mafuriko Mto Ngong yatatiza usafiri kati ya mitaa ya Kayaba na Hazina

Na SAMMY KIMATU

WANAFUNZI na wafanyakazi ni miongoni mwa watu wanaohangaika baada ya daraja moja kusombwa na maji katika Eneo la Viwanda, Kaunti ya Nairobi.

Baada ya mvua kunyesha Jumanne jioni, daraja la Kayaba-Hazina halikupitika kama kawaida baada ya taka ndani ya mto Ngong kuliziba na kusababisha maji kupitia juu yake.

Aidha, usafiri kwa kutumia magari na pikipiki nao ulikatizwa huku madereva wakilazimika kutafuta njia badala kufika ng’ambo ya pili.

Ilibidi vijana kutoka mitaa ya Kayaba na Hazina kujitolea kuwasaidia watu kuvuka mto wakiwatoza ada ya Sh20.

Wakati mmoja, wanafunzi wanne kutoka shule moja ya Msingi mtaani humo waliokuwa wakivukishwa na mwanamume mmoja nusura watumbukie mtoni baada ya kuteleza.

“Ni bahati ya Mungu watoto hao hawakufa baada ya kuteleza walipokuwa wakivuka katika daraja,” Bw Rodriques Lunalo akasema.

Kufikia Jumatano asubuhi, maji yalikuwa yakipitia juu ya daraja bila kuonyesha dalili ya kupungua.

Biashara ya kuvukisha watu ilinonga kwa kundi moja la vijana takriban kumi waliochuma pesa kutoka kwa wateja wao.

Isitoshe, walikuwa wakiwapatia wanaovuka viatu aina ya magwata – Gumboots –  na kuwasaidia kuvuka wakiwashika mikono.

Wengine waliamua kuwabeba watu mgongoni mradi wavuke ng’ambo ya pili.

Mwendesha pilipiki mmoja alifanya kazi ya ziada Jumanne usiku alipotumia bodaboda yake kuwavusha watu akiwatoza ada ya Sh20.

Mnamo mwezi Aprili 2021, kilichokuwa kivukio cha wanaotembea kwa mguu kiliporomoka baada ya kusombwa na maji ya mafuriko.

Usiku huo, vijana wawili walisombwa na maji baada ya daraja kuvunjika wakiwa juu yake kabla ya kutumbukia ndani ya mto Ngong uliojaa pomoni.

“Watu wawili walisombwa na maji wakisaidia watu kuvuka usiku huo baada ya mvua kubwa kunyesha upande wa juu kutoka Milima Ngong na maeneo ya Kibera. Maji mengi mtoni yalishuhudiwa siku hiyo baada ya bwawa la Kibera kupasuka,” mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were akaambia Taifa Leo.

Mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alithibitisha vijana wawili waliokuwa juu ya daraja la Kayaba-Hazina walitumbukia mtoni baada ya daraja kuvunjika na kufunikwa nalo ndani ya mto.

Bw Odingo alikariri kwamba mwanamume mmoja alikufa maji na mwili wake ukaopolewa katika mtaa wa Donholm ulioko zaidi ya kilomita tano kutoka eneo la mkasa.

“Kufikia leo, mwili wa mwanamume wa pili haujapatikana tangu siku ya mkasa huo ulipotokea katikati ya Aprili 2021,” Bw Odingo akanena.

Kando na hayo, serikali ilikuwa imepanga kujenga kivukio kingine cha wanaotembea kwa mguu kwa gharama ya Sh24 milioni.

Hata hivyo, viongozi kwenye tarafa la South B walitoa pendekezo kusitishwa kwa daraja hilo na kusema mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara mpya ya Hazina/Kayaba apewe kazi ya kujenga daraja lingine.

“Baada ya serikali kutumia pesa za umma mara mbili, ni bora wajenge daraja la watu kuvukia na magari kupitia kwa pamoja ndiposa waokoe pesa za walipa ushuru,” Bw Herman Azangu, mwakilishi wa wadi ya Landi Mawe akaambia wanahabari.

Kivukio kilichosombwa na maji kilijengwa miaka ya 90 na aliyekuwa mbunge wa Makadara Bw Reuben Ndolo.

Kabla ya kuingia ulingoni wa siasa, Bw Ndolo alijenga darala la Kayaba-Hazina miongoni mwa daraja nyingine nne.

Wakati huo, Bw Ndolo alikuwa rais wa Baraza la Wanandondi wa nchi zilizo wanachama wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth World Boxing Council-CWBC).

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Sharon Nafula Wekesa

KNUN yadai wazo la kuruhusu matatu kubeba asilimia 100 ya...