• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 3:36 PM
Makanisa yatoa onyo kuhusu ghasia 2022

Makanisa yatoa onyo kuhusu ghasia 2022

VIONGOZI wa makanisa wameonya kuhusu uwezekano wa ghasia baada ya uchaguzi mkuu ujao kwa sababu ya taharuki za kisiasa zinazoendelea kushuhudiwa nchini.

Kupitia kwa Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kenya (NCCK) tawi la Pwani, viongozi hao walisema mijadala kama vile ya kuahirisha uchaguzi hadi marekebisho ya katiba yafanywe, na wanasiasa kuleta mgawanyiko kati ya maskini na matajiri ni hatari kwa amani ya nchi.

Mwenyekiti wao, Askofu Peter Mwero, alionya kuwa jaribio lolote la kukiuka katiba kwa manufaa ya kibinafsi ya wanasiasa linaweza kuzua ghasia.“Wakati huu taifa linapojiandaa kwa uchaguzi, hatuwezi kusahau matatizo ambayo ghasia za uchaguzi zilisababishia wananchi katika miaka iliyopita.

Hatutaki kurudia hali hiyo tena,” akasema Dkt Mwero, ambaye ni Askofu wa Kanisa la PEFA.Kwa wiki chache sasa, mdahalo umekuwa ukiendelea kuhusu pendekezo la baadhi ya viongozi wanaounga mkono marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kwamba uchaguzi wa 2022 usifanyike hadi baada ya refarenda.

Mchakato wa BBI ulipigwa breki mahakama ilipoamua ulikiuka katiba.Kikatiba, Uchaguzi Mkuu huwa wastahili kufanyika katika Jumanne ya pili ya Agosti, kila baada ya miaka mitano. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), tayari imeratibu Agosti 9, 2022 kama tarehe ambapo uchaguzi ujao utafanywa.

Askofu huyo pia alikashifu viongozi wanaojaribu kusababisha mgawanyiko kati ya maskini na matajiri katika jamii wanapojipigia debe akisema huo ni uchochezi hatari sawa na migawanyiko ya kikabila na kidini.Aliitaka Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC), kamati ya kitaifa ya kudumisha amani na kusuluhisha mizozo, IEBC na idara ya polisi kushirikiana na wadau wengine kama vile makanisa ili kueneza umoja wa wananchi.

“Tusisubiri hadi wananchi wachochewe kuzua fujo kabla tuchukue hatua. Ikiwa hatutakomesha mienendo hii sasa, kuna uwezekano mkubwa Uchaguzi Mkuu wa 2022 utakumbwa na ghasia,” akasema.Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika kikao cha wanahabari baada ya kongamano katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kaunti ya Kilifi.

Walitoa wito kwa makanisa kukoma kuwapa wanasiasa nafasi ya kupiga kampeni ndani ya makanisa.Kasisi Ephraim Mbugua wa kanisa la PCEA, alisema wanasiasa wanapoenda kanisani wanafaa wawe kama waumini wengine wote.

“Wanasiasa wanaweza kuja kanisani kama muumini mwingine yeyote, watoe zaka na sadaka ambazo hatufai kutangaza wazi, kisha waende nyumbani. Hawafai kutumia pesa zao kuchafua mimbari,” akasema Bw Mbugua.

  • Tags

You can share this post!

Vinara wa NASA wawakanganya wafuasi wao

Kiini cha 154,524 kutaka nafasi Nanyuki School