• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Maseneta wa Azimio watishia kuvuruga ajenda za serikali katika Seneti

Maseneta wa Azimio watishia kuvuruga ajenda za serikali katika Seneti

NA COLLINS OMULO

MASENETA wa Azimio sasa wanapanga kusambaratisha ajenda zote za serikali ya Kenya Kwanza zitakazowasilishwa katika seneti hadi Spika Amason Kingi atakapoidhinisha mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa na mrengo huo.

Maseneta hao ambao wamekuwa wakisusia vikao vya bunge hilo kwa majuma matatu yaliyopita, wameshikilia kuwa wataendelea kuvuruga vikao vya seneti vinavyorejelewa leo Jumanne alasiri.

Viongozi hao wa upinzani wanamsuta Bw Kingi kwa kuendeleza ajenda za kisiasa katika mvutano huo ambao umekotoka tangu Februari.

Hata hivyo, maseneta wa Kenya Kwanza wamewataka wenzao wa Azimio kudiriki kujaribu kuvuruga shughuli za seneti wakisema hawana idadi tosha ya kufanikisha lengo hilo.

Seneta wa Nairobi na kiranja mteule wa wachache Edwin Sifuna alisema fujo za maseneta wa Azimio, zilizochelewesha kupitishwa kwa Taarifa ya Kisera ya Bajeti (BPS) na taarifa kuhusu mikakati ya kudhibiti madeni (MTDMS) kwa wiki kadha na “hali hiyo itaendelea hadi utata kuhusu mabadiliko ya uongozi wa mrengo wetu utakaposuluhishwa.”

Bw Sifuna ambaye ni Katibu Mkuu wa ODM alisema sehemu ya mkakati huo ni wao kususia mijadala kuhusu ajenda za serikali kwa lengo la kusambaratisha zile ambazo zinahitaji kupitishwa na angalau thuluthi mbili za idadi jumla ya maseneti.
Aliongeza kuwa kupitishwa kwa shughuli muhimu za seneti kunahitaji uungwaji mkono kutoka angalau maseneta 24 waliochaguliwa.

“Kando na ajenda zinazohitaji uungwaji mkono wa thuluthi mbili ya maseneta, yaani maseneta 48 kati ya 67, pia tutasua ajenda zile ambazo zinahitaji kupitishwa na angalau maseneta 24 waliochaguliwa,” Bw Sifuna akaeleza.

Alisema mgomo huo wa maseneta wa Azimio utachangia kuchelewa kupitishwa kwa taarifa mbili muhimu ambazo ziliwasilishwa na mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Bajeti ya Fedha, seneta wa Mandera Ali Roba.

“Tutafanya kila tuwezalo, kadri ya uwezo wetu. Tuko tayari kukaza kamba hadi utulivu urejee katika seneti. Tunataka kutoa ujumbe kwamba seneti ni bunge ambapo maamuzi ya wanachama yanapasa kuheshimiwa. Kwa hivyo, hadi suala hili lisuluhishwe kwa njia inayoridhisha, shughuli za seneti hazitaendeshwa kwa njia ya kawaida,” akasema Bw Sifuna.

“Shughuli nyingi katika seneti zitatuhitaji kwa sababu idadi hitaji lazima ifikiwe na kura ipigwe. Sote, tulioko upande wa wengi na wachache ni muhimu katika kufanikisha shughuli za bunge hili,” akaongeza.

Kauli ya Bw Sifuna iliungwa mkono na mwenzake wa Vihiga Godfrey Osotsi akisema Spika Kingi “ameonyesha kuwa kuwa haheshimu upande wa walio wachache.”

  • Tags

You can share this post!

Diwani aikumbusha serikali ya kaunti ikamilishe ujenzi wa...

CHARLES WASONGA: Wanawake waige ujasiri wa Mama Grace...

T L