• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:59 AM
Mashirika ya kutetea haki yamkemea Kindiki

Mashirika ya kutetea haki yamkemea Kindiki

HILARY KIMUYU Na VICTOR RABALLA

CHAMA cha Wanasheria Nchini (LSK) na mashirika mawili ya kutetea haki yamemkemea Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki kwa kuendelea kutetea polisi waliotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

Kwenye taarifa, LSK, shirika la kutetea haki la Amnesty International-Kenya na Chama cha Matabibu nchini (KMA) walimsuta Waziri kwa kuangazia zaidi thamani ya mali iliyoharibiwa wakati wa maandamano hayo yaliyoitishwa na Upinzani badala ya watu waliouawa na polisi.

Mashirika hayo yalisema kuwa watu 10 waliuawa, 107 wakajeruhiwa na polisi wakiwemo 47 waliopata majeraha ya risasi, hasa katika miji ya Kisumu na Kisii.

“Tunasikitika kuripoti kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha angalau watu 10 waliuawa kwa risasi, wengine wengi wakajeruhiwa kwa risasi na baadhi yao wakapigwa kwa vifaa butu,” mashirika hayo yakasema.

Kulingana na Rais wa LSK Eric Theuri, polisi walionekana kulenga watu kutoka jamii fulani na hasa vijana walipokuwa wakikabiliana na waandamanaji.

“Ripoti zilisema kuwa polisi waliwashambulia kwa risasi waandamanaji ambao hawakuwa na silaha hatari, isipokuwa mawe. Aidha, maafisa hao waliwashambulia watu ambao walikuwa wakitoroka,” akasema.

Bw Theuri alisema polisi hawafai kutumika kama vyombo vya kuendesha vita vya kisiasa kwani nchi inaonekana kurejelea katika enzi ambapo polisi walikuwa wakidharau Katiba.

“Ni makosa kwa polisi kutumiwa kutekeleza unyama dhidi ya raia wasio na hatia kutokana na sababu za kisiasa. Kwa mfano, katika kaunti ya Kisumu polisi walionekana wakivunja nyumba za watu na kuwashambulia kwa marungu na risasi,” akasema.

LSK, Amnesty na KMA pia ziliitaka Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) kukamilisha uchunguzi wa visa vya polisi kutumia nguvu kupita kiasi katika kaunti za Kisumu, Kisii, Homa Bay, Makueni, Nairobi, Migori miongoni mwa nyingine.

“Wahanga wa ukatili wa polisi sharti watendewe haki kwa mujibu wa sheria. Polisi ambao watakapatikana na hatia ya kutumia nguvu kupita kiasi sharti watambuliwe na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria pamoja na makamanda wao,” akasema Bw Irungu Houghton, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Amnesty International-Kenya.

Mashirika hayo yalisema hayo siku moja baada ya Waziri Kindiki kufichua kuwa mali ya thamani ya Sh20 milioni iliharibiwa katika maandamano ya miezi mitatu mjini Kisumu.

Kwenye taarifa kwa seneti Bw Kindiki alisema kuwa wahalifu fulani walijicha ndani ya waandamanaji kupora na kuharibu mali ya umma na ya watu binafsi.

Alisema polisi walifanya kazi yao kwa utaalamu mkubwa zaidi katika jitihada zao za kulinda mali na maisha ya Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Kibera Girls na Soccer Assassins vitani kutafuta mshindi wa...

AMINI USIAMINI: Kakakuona humeza mawe iwe rahisi chakula...

T L