• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Kibera Girls na Soccer Assassins vitani kutafuta mshindi wa Divisheni ya Kwanza

Kibera Girls na Soccer Assassins vitani kutafuta mshindi wa Divisheni ya Kwanza

NA TOTO AREGE

KIBERA Girls Soccer watashuka dimbani Jumapili dhidi ya Soccer Assassins katika mechi ya kutafuta mshindi wa jumla wa Ligi ya Wanawake ya Divisheni ya Kwanza katika uwanja wa RVIST, Kaunti ya Nakuru.

Kibera ilimaliza kileleni mwa Zoni A kwa alama 59 huku Assassins ikimaliza kidedea Zoni B kwa kuzoa alama 46.

“Mechi hiyo pia itatusaidia kujiandaa kwa mashindano ya Kitaifa ya Michezo ya Shule za Upili wiki ijayo,” kocha mkuu wa Assassins Nickson Mileri alisema.

Katika mechi nyingine ya mchujo katika uwanja uo huo, Uweza Women ya Zoni A na Bungoma Queens ya Zoni B zitamenyana katika pambano la kutafuta nafasi ya tatu.

Kocha msaidizi wa Bungoma Jairus Misiko atachukua nafasi ya kocha Robert Majio ambaye anaugua.

“Tulijipanga kusafiri mapema Jumamosi asubuhi ili wachezaji wapate mapumziko ya kutosha. Pia tuliwataka kufahamu eneo la kucheza tofauti na wakati wa ligi ambapo tunafika na kwenda moja kwa moja uwanjani kucheza. Wachezaji wangu wako katika hali nzuri na tuna matumaini ya kuandikisha ushindi kwenye mechi hiyo,” alisema Misiko.

Timu hizo mbili zitakutana kwa mara ya kwanza tangu zijiunge na ligi hiyo.

Timu itakayoshinda itakuwa ya tatu kupandishwa daraja moja kwa moja hadi Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) kuchukua nafasi za Kangemi Ladies, Kisumu All Starlets na Kangemi Ladies ambazo zilishuka daraja msimu jana.

Kibera walimaliza katika nafasi ya tatu katika Kombe la Wanawake la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo mnamo Juni 4, 2023. Waliilaza Kisumu All Starlets 4-2 na kutunukiwa nishani ya Shaba na Sh150,000.

Timu hiyo ilipata tiketi ya kujiunga na KWPL msimu wa 2021/22 lakini ligi hiyo ikatangazwa kubatilishwa na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Kibera na Assassins watarejea nyumbani na Sh500,000 kila mmoja. Mshindi wa jumla wa ligi atatunukiwa kombe kwa hisani ya FKF.

Timu 15 tayari zimeshuka daraja kutoka Daraja la Kwanza katika msimu uliomalizika hivi punde.

Katika Zone A, Solasa Stima Queens, Gusii Starlets FC, Vihiga Leeds FC, Rongai Eaglets FC, Kimathi Lionesses FC, Bomet Starlets, Nyuki Starlets FC na Oserian Ladies zimeshushwa daraja.

Kwingineko katika Zone B, Macmillan Queens, Coast Starlets, Makolanders, Mukuru Talent Academy, Fortune Ladies, Murang’a Queens na Limuru Starlets walifuata mkondo huo.

Mshambulizi wa Assassins Valerie Nekesa ndiye Mshindi wa Kiatu cha Dhahabu 2022/23 akiwa na mabao 37 katika mechi 22. Aliisaidia timu yake kupandishwa daraja hadi daraja la juu kwa mara ya kwanza katika historia.

Katika mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Kimathi Lionesses katika uwanja wa Madira Girls mnamo Julai 29, 2023, Nekesa alifunga mabao 13 katika ushindi wao mnono wa 28-0.

Mshambulizi wa Mombasa Olympic Happy Muta, aliibuka wa pili akiwa na mabao 28.

Winnie Gwatenda wa Kibera alitikisa nyavu mara 23 huku Calta Wanjala wa Falling Waters Barcelona akifuzu kwa nne bora akiwa na mabao 14.

Msimu ujao, ligi ya Divisheni ya Kwanza itachezwa kwa kategoria za Zoni A na B zenye timu 12 kila upande.

  • Tags

You can share this post!

Waiguru na Wangui Ngirici wazika tofauti zao

Mashirika ya kutetea haki yamkemea Kindiki

T L