• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Mbunge azishangaa hospitali za umma kusema hazina mitungi ya Oksijeni

Mbunge azishangaa hospitali za umma kusema hazina mitungi ya Oksijeni

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kiminini Chris Wamalwa amemsuta Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kufuatia tangazo lake Jumatatu kwamba hospitali za umma hazina mitungi ya hewa ya Oksijeni ya kutosha.

Bw Wamalwa alisema Jumanne kauli ya aina hiyo inaashiria utepetevu uliopo katika idara ya afya, kuangazia masuala muhimu kipindi hiki vituo vya afya vinahitajika.

Bw Kagwe alinukuliwa akihimiza wagonjwa wa virusi vya corona walio na mitungi ya hewa ya Oksijeni kuirejesha, Wamalwa akitaja matamshi hayo kama “mzaha wa hali ya juu”.

Mbunge huyo alieleza kushangazwa kwake na jinsi vituo vya afya vya umma vinavyomilikiwa na kufadhiliwa serikali vinaweza kukosa vifaa hivyo muhimu.

“Kwa sasa hospitali za umma hazipaswi kuwa zikitumia mitungi ya Oksijeni. Teknolojia inaendelea kukua, na vituo hivyo vya afya vinapaswa kukumbatia mfumo wa sasa – matumizi ya mifereji iliyosindikwa hospitalini kupitisha Oxijeni kwa kutumia mashine. Hospitali za kibinafsi zimepiga hatua mbele, ilhali hazina fedha vile kama serikali,” akaelezea mbunge huyo, akimtaka Waziri Kagwe kutathmini suala hilo.

Bw Wamalwa alisema ni jambo la kuatua moyo hospitali za umma zikikosa Oksiijeni, kipindi hiki wagonjwa wa Covid-19 wanazidi kufurika humo wakitafuta huduma za matibabu.

Waziri Kagwe aliwarai wagonjwa walio na mitungi ya Oksijeni kuirejesha mara moja, ili kusaidia wenye mahitaji ya dharura.

Ongezeko la visa vya maambukizi ya corona linazidi kushuhudiwa, licha ya Rais Uhuru Kenyatta mwishoni mwa juma lililopita kukaza kamba sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia msambao.

You can share this post!

Mama Sarah Obama azikwa katika hafla iliyohudhuriwa na...

Nike yafika mahakamani kushtaki kampuni kuhusu ‘viatu...