• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
Mfanyakazi wa hospitali ya Mama Lucy Kibaki asukumwa jela miaka 35 kwa kuuza watoto

Mfanyakazi wa hospitali ya Mama Lucy Kibaki asukumwa jela miaka 35 kwa kuuza watoto

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mfanyakazi wa idara ya huduma za kijamii katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki jijini Nairobi mnamo Jumatano alifungwa miaka 35 kwa kuuza watoto.

Fred Leparan alifungwa na hakimu mwandamizi katika Mahakama ya Milimani baada ya kumpata na hatia ya kuuza watoto wachanga wa umri wa kati ya siku nane (8) hadi wiki tatu (siku 21).

Leparan alihukumiwa pamoja na mfanyakazi mwenzake katika idara hiyo ya huduma za kijamii hospitalini humo Selina Awuor Adunda.

Selina alitozwa faini ya Sh300,000 ama atumikie kifungo cha miaka sita gerezani akishindwa kulipa faini hiyo.

Selina alipatikana na hatia katika mashtaka matatu ya kupuuza majukumu ya kazi yake.

Akipitisha adhabu dhidi ya Leparan, Bi Esther Kimilu alisema mfanyakazi huyo wa umma alifanya makosa mabaya.

Bi Kimilu alimpata Leparan na hatia katika mashtaka sita ya kula njama kutekeleza uhalifu, kuuza watoto na kupuuza majukumu yake ya kazi.

“Utatumikia kifungo cha jumla ya miaka 35 kama ifuatavyo. Utatumikia kifungo cha miaka 25 gerezani na miaka 10 utatumikia kifungo cha nje ukipata ushauri nasaha kutoka kwa idara ya urekebishaji tabia,” Bi Kimilu alimweleza Leparan.

Kwa kosa la kula njama za kutekeleza uhalifu, hakimu alimfunga Leparan miaka mitatu.

Leparan alishtakiwa kwamba kati ya Machi 1 na Novemba 16, 2020, katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki akishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa kortini, alikula njama za kushiriki biashara ya ulanguzi wa watu.

Mashtaka ya pili, tatu na nne dhidi ya Leparan yalisema alipokea watoto watatu wa umri wa siku nane, siku 21 na miezi miwili.

Kwa mashtaka haya, hakimu alimhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 kila moja.

“Utatumikia kifungo cha miaka 30 kwa makosa ya kupokea watoto watatu wachanga waliotambuliwa kwa majina J.S (wa umri wa siku 21), NH almaarufu LK (mwenye umri wa miezi miwili) na OM almaarufu AT (mwenye umri wa siku nane),” Bi Kimilu alisema.

Hakimu alifafanua vifungo vitatumika kwa wakati mmoja.

Wote Leparan na Selina walikabiliwa na mashtaka ya kusababisha watoto hao waliokuwa wamewekwa chini ya ulinzi wao kuteseka.

Leparan na Selina walikamatwa kufuatia matangazo yaliyopeperushwa na kituo cha habari cha kimataifa cha BBC kuhusu sakata ya ulanguzi na uuzaji wa watoto.

Wakili Danstan Omari aliyemwakilisha Leparan alieleza mahakama atakata rufaa kupinga adhabu hiyo kali.

  • Tags

You can share this post!

EACC yaenda Bomas kuomba meno

Homa Bay yapata cheti cha utambulisho wa kimataifa kwa...

T L