• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 3:58 PM
Matiang’i aweka mikakati kuzima visa vya wafungwa kutoroka jela

Matiang’i aweka mikakati kuzima visa vya wafungwa kutoroka jela

Na CHARLES WASONGA

ASKARI jela saba wa gereza la Kamiti wamakamatwa kufuatia kisa ambapo wafungwa watatu walitoroka kutoka gereza hilo lenye ulinzi mkali.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatatu usiku baada ya kuzuru gereza hilo, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alisema uchunguzi umebaini kuwa utepetevu wa maafisa hao ndio ulisababisha kutoroka kwa wafungwa hao.

“Maafisa zaidi watakamatwa baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuanzisha rasmi uchunguzi kuhusu kisa hicho,” Dkt Matiang’i akasema.

Waziri alikuwa alitembelea gereza la Kamiti akiandamana na na Katibu katika wizara yake Karanja Kibicho, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, Katibu anayesimamia Idara ya Magereza Zainab Hussein na Mkurugenzi wa DCI George Kinoti. Pia alikuwepo Kamishna Mkuu wa Magereza Wycliffe Ogallo.

Wafungwa watatu waliotoroka na ambao walipatikana na hatia ya ugaidi ni Musharaf Abdalla Akhulunga almaarufu Zarkawi au Alex au Shukri, Mohamed Ali Abikar na Joseph Juma Odhiambo almaarufu Yusuf.

Inadaiwa watatu hao walitoroka kutoka gereza hilo usiku wa kuamkia Jumatatu baada ya kuvunja sehemu ya ua wa ukuta.

Musharaf Abdalla Akhulunga alikamatwa mnamo Septemba 30, 2012 kwa kujaribu kulipua majengo ya bunge.

Mohamed Abdalla Abikar alikamatwa mnamo 2015 kwa kushiriki katika mipango ya mshambulio ya kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa.

Naye Joseph Juma Odhiambo alikamatwa mnamo 2019 katika eneo la Bullahawa, Somalia alipokuwa akienda huko kujiunga na kundi la wapiganaji wa al-Shabaab.

Dkt Matiang’i alisema wizara yake itafanya kila iwezalo kuzuia kisa kama hicho cha kutoroka kwa wafungwa wa uhalifu aina hiyo ambao “wanahatarisha usalama wa raia.”

“Wale ambao watatoa habari zitakazosaidia kukamatwa kwa wafungwa hao ambao ni hatari kwa usalama watalindwa na serikali,” Dkt Matiang’i akasema.

You can share this post!

Maswali wafungwa wa ugaidi wakitoroka jela yenye ulinzi...

SHINA LA UHAI: Saratani ya mapafu: Gharama ya matibabu pigo...

T L