• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
MKU yasifu utaratibu wa kuwaweka waajiriwa katika mkataba wa utendakazi

MKU yasifu utaratibu wa kuwaweka waajiriwa katika mkataba wa utendakazi

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimeweka mkataba wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wote chuoni humo.

Mwenyekiti wa kamati ya chuo hicho, Profesa David Serem alieleza kwamba hatua hiyo ni muhimu kwa sababu inabadilisha mwelekeo wa utendaji kazi wa wafanyakazi chuoni.

“Kwa muda wa miaka miwili tangu tuweke saini makubaliano hayo, wafanyakazi wa hapa chuoni wameonyesha mwelekeo mzuri katika majukumu yao na tuna imani mwelekeo utabaki kuwa ni huo,” alifafanua Prof Serem.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa wakati wa kutia saini mkataba wa maelewano ambao huendeshwa aghalabu kila mwaka.

Naibu Chansela wa chuo hicho Prof Deogratius Jaganyi aliyehudhuria hafla hiyo alisema ni muhimu kwa mpango huo kuendelea.

“Kutiwa saini kwa mpango huo miongoni mwa wafanyakazi wa chuo hiki ni muhimu kwa sababu mpango huo utaboresha utendaji kazi wa kila mwajiriwa,” alieleza Prof Jaganyi.

Profesa Jaganyi alitoa hakikisho kwa wasimamizi wa chuo hicho kuwa mpango huo ni hatua kubwa ya kujivunia na itaweza kuboresha matakwa ya wafanyakazi wote wa chuo hicho kufuatana na ruwaza ya mwaka wa 2020 hadi 2029.

Alieleza kuwa mwaka 2021 mkataba uliotiwa saini na wafanyakazi ulikuwa wa kufana na kuna matumaini ya mazuri mengi kuonekana.

“Mtu mmoja hawezi akafanikiwa akiwa pekee lakini tukiungana pamoja tutafika mbali. Mtu mmoja ni kama tone la maji lakini umoja wetu  ni kama ziwa,” Profesa Jaganyi alisema akinukuu matamshi ya msomi mmoja kwa jina Ryunosuke Satoro.

Baadhi ya wakuu wengine waliohudhuria hafla hiyo ya kutia saini ni Pro-Chansela wa chuo hicho Dkt Vincent Gaitho na mkuu wa utafiti na masomo ya juu Dkt Bibian Waiganjo Aidi.

Dkt Gaitho alisema chuo hicho kinatambua utendaji kazi wa kila mfanyakazi, jambo alilosema limeimarisha ushirikiano mwema miongoni mwao.

  • Tags

You can share this post!

Hofu lishe duni, mihadarati yawageuza vijana goigoi

ICC: Gicheru apumua ombi la upande wa mashtaka likitupwa nje

T L