• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Mkulima hodari anavyotengeneza mbolea asilia

Mkulima hodari anavyotengeneza mbolea asilia

NA PETER CHANGTOEK

HUKU akivalia shatitau jeupe na suruali ndefu nyeusi, Jeremiah Wainaina anakitwaa kitoma cha plastiki, kisichokuwa na kitu chochote ndani, katika kitongoji cha Kithanjeni, katika eneo la Chuka, kisha anakijaza kitoma hicho kwa kimiminika chenye rangi ya njano.

Yeye ni mkulima mwenye uwezo wa kutengeneza mbolea asilia, kwa kuitumia mimea fulani, na amekuwa akitumia mbolea hiyo kuikuza mimea shambani kwake, na hivyo kuondoa gharama ya kuzinunua mbolea za madukani.

“Hii ni Tithonia; mbolea kiowevu ambayo mimi hutengeneza kwa kukusanya majani na matawi, kutoka kwa mmea wa Tithonia. Hukatakata kuwa vipande vidogo vidogo na kuweka kwa mtungi na kufunika na kuweka kwa kivuli kwa muda wa siku 21,” asimulia Wainaina.

Baada ya rangi nyeusi kuonekana kwa kiowevu hicho, hiyo ni ishara kwamba, mbolea hiyo imekuwa tayari. Yeye huchuja ili kuondoa uchafu na baada ya kuchujwa, huwa tayari kwa matumizi. Mbolea hiyo huweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu pasi na kuharibika.

Mkulima huyo, mwenye umri wa miaka 63, huwa hatengenezi mbolea hiyo tu, bali pia hutengeneza mchanganyo fulani unaotumika kuangamiza wadudu na kuzuia maradhi kwa baadhi ya mimea, kama vile mikahawa.

Wainaina akionyesha mbolea asilia kiowevu iliyoko kwa vitoma….PICHA/ETER CHENGTOEK

Wainaina huchanganya pilipili, vitunguu saumu, mkojo wa sungura, pamoja na majani ya mimea tofauti tofauti, ili kutengeneza dawa za kuwaua wadudu.

Anadokeza kuwa, hapo awali, mimea yake ya mikahawa anayoikuza ilikuwa imeanza kuzaa mazao kidogo, lakini baada ya kutumia mbolea hiyo, mimea yake 114, ikaanza kumpa mazao zaidi ya tani moja.

Anaongeza kuwa kwa kila mmea, kwa sasa, huzaa kilo 10 za kahawa, lakini hapo awali, mmea mmoja ulikuwa ukimpa kilo moja tu ya kahawa. Anasema kuwa anendelea kuitunza mimea hiyo, akiwa na matumaini kuwa, kila mmea utakuwa ukimpa kilo 20 za kahawa.

Kwa wakati huu, wakulima kadhaa hufurika shambani kwake, ili kupata mafunzo kuhusu matumizi ya mbolea hiyo, na baadhi yao, vilevile, huinunua ili kuitumia katika mashamba yao. Aidha, yeye hulipwa na wakulima hao kunyunyizia mimea yao mbolea na dawa.

Kwa kuitumia mbolea hiyo, mkulima huyo, anasema kuwa mimea yake mingine, kama vile mboga, hunawiri mno shambani. Pia, ameweza kuwakabili wadudu waharibifu, kwa kuutumia mchanganyo huo wa vitunguu saumu, pilipili, na mkojo wa sungura.

Aliacha kabisa kutumia mbolea za madukani, anazodai zina kemikali hatari, na anazosema zilikuwa zimeharibu rutuba kwa shamba lake, alipokuwa akizitumia.

“Mmea wa Tithonia ni wa kutegemewa kwa kuwa una naitrojeni, potassium na fosiforasi, kwa ajili ya ukuaji wa mimea, na ukosefu wa naitrojeni hufanya mmea kutokua,” asema Wainaina.

Anaongeza kuwa, kuwepo mchangani kwa fosiforasi (phosphorous), husaidia mimea kuwa yenye nguvu, na kuwa na mazao bora. Anaongeza kuwa, kutokuwa na madini hayo mchangani hufanya mimea kukua polepole na kunyauka ovyo.

Wainaina anawashauri wakulima wengine kutumia mbolea asilia. Anasema kuwa, mbolea kiowevu anayoitengeneza, ina virtutubisho vilivyo tayari kufyonzwa kwa urahisi na mimea. Anasisitiza kuwa, mbolea yenyewe huwafukuza wadudu wanaovamia mimea shambani.

Kwa mujibu wa Teresa Ndirangu, mtaalamu katika taasisi ya College of Sustainable Agriculture for Eastern Africa (CSAEA), matumizi ya mboleafunde, husaidia kurutubisha udongo na hivyo kuuwezesha udongo kushikilia maji kwa muda mrefu. Pia, humwezesha mkulima kuwa na mazao mengi.

Mtaalamu huyo anaongeza kwamba, wakulima wanafaa kuikuza mimea tofauti tofauti, na kubadilishabadilisha mfumo wa ukulima, ili udongo uwe na rutuba na magonjwa yasiharibu mimea kwa urahisi shambani.

  • Tags

You can share this post!

Maseneta wakemea wanahabari kwa kuchapisha video waliyodai...

Wanaotegemea vibarua vya ujenzi walia nyongeza ya bei ya...