• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 1:42 PM
Wanaotegemea vibarua vya ujenzi walia nyongeza ya bei ya mafuta kuwakandamiza zaidi

Wanaotegemea vibarua vya ujenzi walia nyongeza ya bei ya mafuta kuwakandamiza zaidi

Na SAMMY WAWERU

WAKENYA wameeleza kukerwa na ongezeko la hivi punde la bei ya mafuta ya petroli ambayo ilianza kutekelezwa rasmi jana.

Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi Nchini (EPRA) ilitangaza Jumanne ongezeko la Sh7.58 kwa petroli, mafuta ya dizeli na ya taa yakipanda kwa Sh7.94 na Sh12.97 mtawalia.

Kufuatia ongezeko hilo, mwananchi wa mapato ya chini na kadri anatarajiwa kuathirika pakubwa gharama ya maisha na uchumi ikizidi kupanda.Wahudumu na wafanyakazi wa sekta ya juakali wamelalamikia nyongeza hiyo, wakisema tayari wameanza kuhisi athari zake.

Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali, Bw Rustus Matia ambaye ni mfanyakazi wa vibarua vya ujenzi Zimmerman, Nairobi, ameeleza kushangazwa kwake na serikali kuongeza bei ya mafuta kipindi ambacho taifa linaendelea kuhangaishwa na Homa ya Corona.

“Asubuhi nikielekea kazini, niligutushwa na nauli kuongezeka kwa Sh20. Ninaishi eneo la Kimbo, Ruiru na kwa kawaida hulipa Sh100 kufika eneo la kazi, ila leo ilikuwa Sh120. Serikali inaendelea kutukandamiza wakati ambapo vibarua tunavyotegemea havipatikani kwa urahisi,” Bw Matia akateta.

Bw Perkins Agola akiendeleza kibarua cha ujenzi eneo la Zimmerman, Nairobi…PICHA/SAMMY WAWERU

Ni baba wa watoto sita, wote wakiwa shuleni na wanamtegemea kwa karo, chakula, matibabu, mavazi na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.“Kwa siku mapato huwa kadri ya Sh1, 500 na vibarua huvipata mara tatu kwa juma.

Mapato hayo mbali na kuwa tegemeo kukidhi familia yangu riziki na mahitaji muhimu, ndiyo kodi ya nyumba ya Sh10, 000,” akaelezea, akishangaa maisha yatakavyokuwa baada ya nyongeza ya jana ya bei ya mafuta.

Awali, Matia alikuwa akitegemea gesi kufanya mapishi na bei yake ilipotathminiwa na kuongezwa, aligeukia makaa na mafuta ya taa.“Tunaishi kwa neema za Mungu tu. Viongozi tuliochagua wamesalia kimya, hatuskii wakitetea Mkenya wa kawaida akiendelea kuumia,” akasema.

Kilio cha mwananchi huyo si tofauti na cha Perkins Agola, ambaye pia hufanya kazi ya mjengo Zimmerman.Bw Agola ana wasiwasi jinsi atakavyomudu kukimu familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu, kupitia ujira wa Sh600 kwa siku.

“Kwa wenye familia, maisha yanazidi kuwa magumu. Kwa mwezi gharama ya kodi ya nyumba na chakula ni Sh6, 500, mshahara ninaopata hautoshi kamwe,” akasema kibarua huyo ambaye ni baba wa watoto watatu, wenye umri wa miaka 12, 7 na 4.

“Karo inatoka kwa ujira ambao nikifanya hesabu, ninaupata kwa majuma mawili pekee kwa mwezi,” Bw Agola akaelezea, akiirai serikali kutathmini bei ya mafuta ya petroli ambayo athari zake zimeanza kuelekezwa kwa bidhaa za kula na nauli.

Kufuatia mwongozo wa EPRA, petroli sasa inauzwa Sh134.72 kwa lita jijini Nairobi na viunga yake.

Lita moja ya dizeli jijini inagharimu Sh107.66 na mafuta taa ambayo hutegemewa na Wakenya wenye mapato ya chini ikiuzwa Sh110.82, kila lita.

  • Tags

You can share this post!

Mkulima hodari anavyotengeneza mbolea asilia

Wizara ya Kilimo inavyoshirikisha vijana na kuwapa motisha...