• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Msako: Polisi waonja uhuni wa bodaboda

Msako: Polisi waonja uhuni wa bodaboda

MARY WANGARI, BRIAN OJAMAA, WANGU KANURI

TABIA ya uhuni na kujichukulia sheria mikononi imezidi kujitokeza wazi miongoni mwa waendeshaji pikipiki siku chache tu baada ya kundi la wanabodaboda kumdhulumu mwanamke katika kisa kilichoibua hisia kali.

Waendeshaji bodaboda hao wameonyesha ukaidi wa hali ya juu wa sheria kwa kuwashambulia maafisa wa polisi wanaofanya msako kuwakamata wale wanaovunja sheria kufuatia agizo lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta Jumanne.

Katika eneobunge la Kabuchai, Kaunti ya Bungoma, maafisa wa polisi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya waendeshaji bodaboda waliokuwa wakiwarushia mawe wakati wa msako unaoendelea.

Maafisa hao wa kulinda usalama walikabiliana vikali wakikimbizana na wahudumu wa bodaboda waliokuwa wakikataa kukamatwa.

Wana bodaboda hao kisha walianza kuwarushia mawe maafisa hao waliojihami na kuwalazimu kufyatua risasi hewani.

Vioo vya gari la Mbunge wa eneo hilo Majimbo Kalasinga vilipasuliwa wakati wa kisa hicho.

Mbunge huyo alijikuta kwenye ghasia hizo alipokuwa akielekea katika Kituo cha Polisi cha Chwele kuwasihi maafisa wa polisi kuwaachilia huru wanabodaboda waliokamatwa.

Aliwarai waendeshaji bodaboda kukoma kuchukua sheria mikononi mwao akisikitika kuwa tabia hiyo ya uhuni inaifanya serikali kuwachukulia hatua kali.

“Walipiga mawe gari langu ilhali nilikuwa ninaenda kuwasaidia. Sasa nimelazimika kupeleka gari langu gereji,” alisema Bw Majimbo.

Katika kaunti ya Nairobi, operesheni ya kuondoa bodaboda katika jiji kuu ilishika kasi ambapo kufikia jana maafisa wa polisi walikuwa wamenasa zaidi ya pikipiki 125 zilizozuiliwa katika kituo hicho.

Kulingana na Kamanda wa Polisi (OCPD) katika Kituo cha Starehe Central, Nairobi, David Mburukua, operesheni hiyo iliyoanzishwa juzi itaendelea hadi serikali itakaposema vinginevyo.

“Operesheni hii ni kama funzo kwa waendeshaji bodaboda ambao baadhi yao wamekuwa wakitekeleza uhalifu pamoja na kukiuka sheria za barabara,” alisema Bw Mburukua.

Waziri wa Usalama wa Ndani amewapa waendeshaji bodaboda muda wa siku 60 kujisajili kwa Sacco. Katika kaunti ya Narok, wanabodaboda hao waliomba waruhurumiwe ili wasikose riziki.

Naye mwenyekiti wa chama cha wanabodaboda kaunti ya Machakos, Allan Musembi alisisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mwanachama kuwa na beji ya kujitambulisha na kila mmoja kuwa mwanachama wa kituo anachotambuliwa na wenzake.

Alisema hatua hii itasaidia kukabiliana na visa ya uhalifu.

Katika kaunti ya Kisumu, polisi walilazimika kuwakimbiza wanabodaboda waliokataa kusimama wakati wa msako.

Haya yamejiri huku waendeshaji bodaboda katika kaunti hiyo wakihimizwa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri usalama kwa sababu wanachangia nafasi muhimu kama wapiga kura.

Wahudumu hao wameshauriwa kujisajili katika vyama vya Akiba na Mikopo (SACCO) na kupata leseni mpya za kidijitali ili kuepuka kukamatwa.Aidha, maafisa wa usalama wamewaonya dhidi ya kutumiwa na wanasiasa kusababisha vurugu.

HABARI ZAIDI NA KNA

You can share this post!

Mbio za vigari za Karting yavutia madereva 8 wapya

Raila aitwa kuhojiwa NCIC kwa kusema hataki...

T L