• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Mshtuko jamaa ‘aliyezikwa’ akijitokeza

Mshtuko jamaa ‘aliyezikwa’ akijitokeza

NA SHABAN MAKOKHA

FAMILIA moja katika Kaunti ya Kakamega imekumbwa na mshtuko baada ya kuzika mwili wa mtu mwingine kimakosa ikifikiri ni ‘jamaa yao aliyekufa.’

Hali ya sintofahamu iligubika familia ya Bw Joseph Wemali Alucheri kutoka kijiji cha Shamsinjiri, aliyeaminiwa kuuawa na mwili wake kutupwa katika Mto Yala.

Familia hiyo ilichukua mwili kutoka mochari ya Yala ikidhani ni mwana wao kabla ya kuandaa mazishi ambayo kama kawaida yalivutia jamaa wa familia, majirani na kanisa.

Dada yake ‘marehemu’ Bi Everline Ayieta, alisema walisikia ripoti kuhusu mwili ulioanza kuoza uliotolewa Mto Yala na wakaelekea kwenye mochari hiyo.

“Maelezo yalilingana na kaka yetu aliyetoweka kwa hali ya kutatanisha. Tulielekea mochari na mama yetu aliyeandamana na kaka zake walio wajomba zetu lakini tukatofautiana katika kuutambulisha mwili kama wa kaka yangu – Alucheri. Tulichukua mwili na kupanga mazishi huku baadhi yetu wakiwa na shaka,” alisema Bi Ayieta.

Hata hivyo, kijiji hicho kilipigwa na bumbuwazi baada ya ibada ya mazishi ilipogunduliwa kuwa mwanamme aliyeaminiwa kufa yu hai na alikuwa amezuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Khwisero.

Baada ya mazishi familia ilipokea ripoti kuwa jamaa yao waliyemzika yupo hai jijini Nairobi.

Familia hiyo sasa inamlaumu mama yao na wajomba kwa kushindwa kuutambua mwili wa mwana wao na kusisitiza kupatiwa mwili usiofaa.

Bi Ayieta alisema waligombana katika mochari wakati jamaa wengine walikana mwili huo lakini mama na wajomba zao wakasisitiza ni wa Alucheri.

“Tulipata hasara kubwa kusafirisha mwili. Tulilipa zaidi ya Sh30,000 kukamilisha mchakato wa kuuleta mwili na kupanga mazishi yake. Tunataka wajomba zetu warejeshe hela hizo kwa sababu walichukua sehemu ya pesa hizo,” alisema.

Mzee wa kijiji, James Omutula, 86, alisema watafanya tambiko litakalohusisha kuchinja kondoo na kuku.

“Matumbo ya kondoo yatatumika kuondoa mapepo katika mwili usiofaa ulioletwa nyumbani,” alisema Bw Omutula.

Alisema nyumba ya Bw Alucheri, ambapo mwili uliwekwa kabla ya kuzikwa itabomolewa.

“Hatuwezi kumruhusu (Alucheri) kutumia nyumba hiyo hiyo.”

Familia hiyo jana ilifika katika Mahakama ya Butere kuomba idhini ya kuufukua mwili uliozikwa na kuurejesha kwenye mochari.

Kamanda wa Polisi katika Kituo Kikuu cha Kakamega, Valerine Obare, alisema mwili huo unaweza kufukuliwa tu kupitia amri ya mahakama.

“Kwa sasa, hakuna jambo jingine linaloweza kufanywa hadi mahakama itakapotoa amri ya kuufukua mwili,” alisema.


  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Mradi walenga kuokoa wanawake ukiangazia...

MCA ataka Mbarire aeleze hatima ya waliopewa likizo

T L