• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Mudavadi alivyosaliti wenzake OKA

Mudavadi alivyosaliti wenzake OKA

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, aliwapumbaza vinara wenza katika One Kenya Alliance (OKA) kwa takriban miaka miwili huku akiendeleza mazungumzo ya chini ya maji na Naibu Rais William Ruto hadi Jumapili iliyopita, walipotangaza ushirikiano wao.

Hii ni baada ya kuibuka kuwa alianza kuzungumza na Dkt Ruto kwa siri hata kabla ya kubuniwa kwa OKA. Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Benjamin Washiali ambaye ni mshirika wa Dkt Ruto, amefichua kuwa mazungumzo hayo yalianza 2020 ilhali muungano wa OKA ulibuniwa mwaka 2021.

Wadadisi wanasema kwamba kuna uwezekano Bw Mudavadi alikuwa fuko wa Dkt Ruto sio tu katika OKA bali pia katika mipango ya siasa za urithi ya watu wenye ushawishi serikalini kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

OKA ulioleta pamoja Bw Mudavadi, Kalonzo Musyoka(Wiper), Moses Wetangula ( Ford Kenya) na Gideon Moi ( Kanu) , ulikumbwa na madai ya usaliti na kutoaminiana kutoka kwa washirika wa Bw Mudavadi yaliyothibitishwa Jumapili na tangazo la Bw Mudavadi la kuungana na Dkt Ruto.

Bw Musyoka na Bw Moi waliondoka Bomas of Kenya ambapo Mudavadi alikuwa akizindua rasmi azma yake ya kugombea urais, walipogundua alikuwa amealika Dkt Ruto na washirika wake katika chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Washirika wa Bw Musyoka na Bw Moi wanasema kuwa, ingawa hawakufahamu kuwa Bw Mudavadi alikuwa amealika Dkt Ruto na washirika wake katika hafla ya kuzindua azma yake, walikuwa wakishuku kujitolea kwake katika OKA.

Hii ni kwa sababu washirika wake walikuwa wakisisitiza kuwa lazima jina lake litakuwa kwenye debe na kwamba ndiye alitosha kupeperusha bendera ya OKA.

“Mudavadi alisaliti vinara wenzake katika OKA kwa kuunda muungano mwingine na UDA,” alisema Katibu Mratibu wa chama cha Wiper, Bw Robert Mbui.

Usaliti huo ulianza kubainika kutokana na matamshi ya washirika wake wakiongozwa na Seneta wa Kakamega Cleopas Malala ambao walikuwa wakidunisha vinara wengine katika OKA.

“Tulitilia shaka kujitolea kwake katika OKA hasa baada ya washirika wake kuanika ukuruba wao na Dkt Ruto katika mechi ya soka Mumias na katika mkutano mmoja mjini Eldoret. Kile ambacho hatukuwa na hakika ni kina cha mazungumzo yao hadi alipokosa kuhudhuria mkutano uliopaswa kutoa mwelekeo kuhusu mgombea urais wa OKA,” akasema mbunge mmoja wa chama cha Wiper ambaye aliomba tusitaje jina kwa kuwa sio msemaji rasmi wa muungano huo au chama chake.

Msemaji wa chama cha Kanu, Bw Fred Okango, alisema kwamba hatua ya Bw Mudavadi haikuwashangaza japo hawakutarajia angeungana na Dkt Ruto.

“Amechagua kuungana na maadui wetu na kwa hivyo nasi tumeamua kucheza kivyetu na kuchukua mwelekeo tunaohisi utafaidi nchi,” alisema Bw Okango.

Akizungumza Jumatatu katika hafla moja eneo la Mwingi, Bw Musyoka alitaja kujiondoa kwa Mudavadi katika OKA kama kuondoa msongamano katika safari ya kuelekea ikulu.

“Naweza kusema kuwa msongamano umeondoka na sasa njia iko shwari,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Kigame kuzindua muungano

Uhuru ajibu mishale ya Ruto Magharibi

T L