• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Muthama, mkewe wa zamani waanza kuraruana kisiasa

Muthama, mkewe wa zamani waanza kuraruana kisiasa

Na WAANDISHI WETU

ALIYEKUWA Seneta wa Machakos, Johnstone Muthama na mkewe wa zamani Agnes Kavindu, walijibizana wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa useneta kaunti hiyo ziliposhika moto Jumanne.

Akihutubu katika kituo kikuu cha magari ya umma cha Machakos, Bw Muthama alikosoa Chama cha Wiper akisema Bi Kavindu hana uwezo wa kuongoza kaunti katika seneti.

“Wiper ilichagua mtu ambaye hana uwezo wala ujasiri unaohitajika kutetea masilahli ya wakazi wa Machakos,” akasema.

Akimjibu, Bi Kavindu anayewania wadhifa huo kupitia Wiper alimwomba waheshimiane katika kampeni.

“Mwanamke anafaa afanyeje baada ya kufukuzwa nyumbani na mume wake? Je, mtu anafaa kufa tu baada ya talaka?” akauliza katika uwanja wa Mulu Mutisya, akaomba masuala yao ya ndoa yasiingizwe katika kampeni.

Kauli za viongozi mbali mbali walioandamana na wagombeaji hao zilionyesha uchaguzi huo utakuwa wa kupima ubabe kati ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa kaunti hiyo Alfred Mutua na aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo Johnstone Muthama.

Kiti hicho kilibaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa seneta Bonface Kabaka. Uchaguzi mdogo utafanyika Machi 18.

Kuanzia Jumanne wagombeaji wa vyama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto, Maendeleo Chap Chap cha Gavana Mutua na Wiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka wamekuwa piga kambi mjini Machakos.

Bw Mutua anawarai wakazi kumpigia kura mgombeaji wa chama chake Bw Mutua Katuku akisema ni mwanasiasa mkomavu na mwenye uzoefu.

Bw Katuku ni mbunge wa zamani wa eneo la Mwala na alihudumu kama waziri wa maji.

“Nipatieni seneta aliye na uzoefu wa miaka mingi anisaidie kufanya maendeleo haraka badala ya kunisumbua,” Dkt Mutua aliwaambia wakazi baada ya Bw Katuku kuidhinishwa na IEBC.

Aliwapuuza wapinzani wanaosema ni makosa kwa gavana na seneta kutoka chama kimoja.

Viongozi wa Tangatanga walidai kwamba kupigia kura mgombeaji wa Maendeleo Chap Chap au wa Wiper ni kuchagua BBI ambayo walidai haina cha kuwafaidi Wakenya masikini.

Naye Bw Musyoka alisema Bi Kavindu ndiye anayeelewa shida za wakazi wa kaunti ya Machakos.

Alisema kwamba ushindi wa Wiper katika uchaguzi huo utaimarisha nafasi ya kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Musyoka aliungana na viongozi wa vyama vya kisiasa wanaounga BBI, Musalia Mudavadi (Amani National Congress) Moses Wetangula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) kumpigia debe Bi Kavindu akisema ndiye anayeelewa shida za wakazi wa kaunti ya Machakos.

Kuandamana kwa viongozi hao katika kampeni kulichukuliwa na baadhi ya wadadisi kama ishara ya uundaji wa muungano mpya wa kisiasa ambao huenda ukatumiwa kwa uchaguzi mkuu ujao 2022.

Chama cha ODM kinachoongozwa na Bw Raila Odinga hakina mgombeaji katika uchauzi huo mdogo.

Ripoti za Pius Maundu, Kitavi Mutua na Benson Matheka

You can share this post!

Kalonzo ajizolea sifa ya tikitimaji

Magufuli adai chanjo ya kigeni imeingiza corona mpya...