• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Muturi na Lusaka wapokea ripoti kuhusu Mswada wa BBI

Muturi na Lusaka wapokea ripoti kuhusu Mswada wa BBI

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka Jumatano walipokea ripoti kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Baada ya kupokea ripoti hiyo Bw Muturi alitoa notisi kwa wabunge kwamba watahitajika kuhudhuria kikao maalum mnamo Jumatano na Alhamisi wiki hii kujadili ripoti kuhusu mswada huo ambapo umeibua hisia kali miongoni mwa wabunge na wananchi.

Bunge la kitaifa pia litajadili mswada huo wa BBI katika hatua zote tatu kisha kuupigia kura.

“Kwa mujibu wa sheria za bunge nambari 29 (3) wabunge na umma wanajulishwa kwamba kutakuwa na kikao maalum cha Bunge la Kitaifa mnamo Jumatano Aprili 28, 2021 na Alhalisi Aprili, 2021 kuanzia saa nne asubuhi na kuanzia saa nane na nusu alasiri,” akasema Bw Muturi katika tangaza kwenye toleo rasmi la gazeti ya serikali.

Bunge la kitaifa pia litajadili marekebisho ambayo Seneti ilifanya kwa Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORB), 2021.

Aidha, Kamati ya Bunge kuhusu Elimu itawasilisha ripoti yake kuhusu upigaji msasa wa Jamleck Muturi John aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) na Timon Oyucho aliyeteuliwa kwa nafasi ya mwanachama wa tume hiyo.

Wabunge pia watajadili ombi la kuondolewa kwa Bi Tabitha Mutemi kama mwanachama wa Baraza la Kusimamia Vyombo vya Habari Nchini (MCK).

Kwa upande wake, Spika Lusaka alisema kuwa atashauriana na Uongozi wa Seneti kuamua ni lini ripoti hiyo kuhusu Mswada wa BBI itawasilishwa katika bunge la seneti ili ijadiliwe.

You can share this post!

Siraj Mohamed sasa atia bidii kuichezea Harambee Stars

Matumaini kaunti ikisaka soko la maembe ng’ambo