• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:15 AM
Nilitamani Raila ashinde urais mwaka 2013 – Issack Hassan

Nilitamani Raila ashinde urais mwaka 2013 – Issack Hassan

NA CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ahmed Issack Hassan hatimaye amefichua kuwa alitamani kwamba Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga angeshinda katika kinyang’anyiro cha urais Machi 2013.

Akiongea wakati wa kipindi cha JKLive kwenye runinga ya Citizen, Jumatano usiku, Bw Hassan alisema kuwa hiyo ni kutokana na uhusiano wa muda mrefu kati yake na Waziri huyo Mkuu wa zamani.

Alisema kiongozi huyo wa Azimio la Umoja-One Kenya alichangia pakubwa kuteuliuwa kwake kuwa kuwa mwenyekiti wa IEBC, licha ya kwamba baadhi ya watu walijaribu kuanza kuvuruga uteuzi wake kuwa mwanachama wa Tume ya Marekebisho ya Katiba.

“Nina heshima kwa waziri mkuu wa zamani na nilipata kazi yangu ya kwanza kama kamishna katika Tume ya Mageuzi ya Katiba, wakati ambapo alikuwa akihudumu kama mwenyekiti wa kamati teule ya bunge kuhusu katiba. Walituhoji na nilikuwa miongoni mwa wale walioteuliwa kutoka Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Namshukuru kwa hili kwa sababu kulikuwa na jaribio la kujaribu kupinga uteuzi huo lakini Raila akakataa,” Hassan akaambia msimamizi wa kipindi cha JKLive, Jeff Koinange.

Aliongeza japo alitaka Wakenya waonje urais wa Bw Odinga, hilo halikufanyika kwa sababu Uhuru Kenyatta (rais mstaafu) ndiye aliibuka mshindi.

Hassan alisema japo ushindi wa Bw Kenyatta ulimvunja moyo, hakuwa na la kufanya kwa sababu “hayo yalikuwa mapenzi ya Wakenya.”

“Kama mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, kazi yangu ni kutangza mapenzi ya wananchi. Ulikuwa wakati mgumu kwangu lakini ningefanya nini?” akauliza.

Baada ya Bw Kenyatta kutangazwa mshindi, Odinga na wandani wake walianza kuishambulia IEBC kupitia maandamano jijini Nairobi, na kushinikiza kung’olewa mamlakani kwa mwenyekiti na makamishna wenzake.

  • Tags

You can share this post!

Madoli ya ngono kuharibiwa na KRA

Rachel Hellen Waithira: Siri ya mafanikio ni kujua...

T L