• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Nyoro ajadiliana na madiwani jinsi ya kufufua miradi iliyokwama Thika

Nyoro ajadiliana na madiwani jinsi ya kufufua miradi iliyokwama Thika

Na LAWRENCE ONGARO

GAVANA wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro alifanya mkutano wa dharura na madiwani wapatao kumi wa kaunti ndogo ya Thika Magharibi na Thika Mashariki ili kupanga mikakati ya kuamsha miradi ya maendeleo iliyokwama kwa muda mrefu.

Wakazi wa maeneo hayo wamekuwa wakitatizwa na maswala mengi ya kimaendeleo na kwa hivyo ilileta mwamko mpya kati ya gavana na madiwani.

Mkutano huo wa saa tano, ulifanyika katika ukumbi wa kaunti ndogo ya Thika huku kila kiongozi akiweka wazi kwa meza ni jambo lipi la dharura lililokuwa muhimu kwao kutatuliwa.

Baadhi ya maswala mengi na ya dharura yaliyozungumziwa ni kuboresha masoko yaliyoko hasa kuzibua majitaka yanayoshuhudiwa kila mara mitaani kunaponyesha mvua.

Wakazi wengi katika mitaa tofauti wamekuwa wakikosa maji safi ya matumizi.

Kumekuwa na maswala ya miundomsingi hasa barabara zinazoingia mitaani, wakazi wakisema haziko katika hali njema na hivyo mkutano huo uliazimia kuona haja ya kuzikarabati.

Gavana Nyoro alisema jambo la muhimu kwa sasa ni kuchapa kazi kwa umoja na ushirikiano bila malumbano ili kukamilisha pia ajenda zilizoafikiwa na kaunti kwa jumla.

“Katika muda wa mwaka mmoja uliosalia kuelekea uchaguzi mkuu tumekubaliana na viongozi wengine kuweka vichwa vyetu pamoja na kutumikia wananchi. Ni lazima tuhakikishe ‘Wanjiku’ anafanyiwa kazi kikamilifu,” alisema gavana huyo.

Alieleza kuwa baada ya siku chache zijazo atakutana na wasimamizi wote wa sekta tofauti ili kuona ya kwamba kazi inatendeka kwa umakini na usawa katika kila wadi.

Bw Raphael Chege ambaye ni MCA wa wadi ya Kamenu alisema aliridhishwa na mkutano huo kwa sababu kila mwakilishi wa wadi alipewa nafasi kujitetea na kutaja shida zinazokumba eneo lake.

“Mimi nimeridhika na mkutano huo kwa sababu nina imani kuwa soko la Madaraka, Makongeni litapata umeme na maji kwa wakati ufaao. Tumekuwa na shida kubwa kwa muda mrefu,” alifafanua Bw Chege.

Alisema mkutano huo ulikuwa na umuhimu wake kwa sababu waliweza kujadiliana kwa uwazi na gavana wao ambaye alionyesha ushirikiano mwema.

Naye diwani maalum wa mji wa Thika Bw Tonny Njiru, alisema mvua ambayo imenyesha kwa zaidi ya mwezi mmoja iliharibu miundo msingi ya maeneo mengi jambo lililosababisha hasara kubwa.

“Tuna imani ya kwamba wananchi watanufaika na mabadiliko yatakayokuja hivi karibuni. Sisi kama viongozi tutajizatiti kuona tunatekeleza wajibu wetu,” alisema Bw Njiru na kuongeza “ni muda tu tungetaka tupewe”.

  • Tags

You can share this post!

Vyoo vya soko la Witeithie vyabomolewa

Corona: Hitilafu ya oksijeni hospitalini yaua watatu